Ndugai ataja mafanikio 15 ya Rais Magufuli

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ametaja mambo 15 aliyofanya Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka minne alichokaa madarakani na kuwataka Watanzania kumuunga mkono.

Moshi. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ametaja mambo 15 aliyofanya Rais John Magufuli kwa kipindi cha miaka minne alichokaa madarakani na kuwataka Watanzania kumuunga mkono.

Ndugai aliyataja mambo hayo jana Mjini Moshi wakati akizungumza kwenye kongamano la kumpongeza Rais lililoandaliwa na Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa Kilimanjaro.

Hotuba ya Ndugai ilisomwa kwa niaba yake na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson katika uwanja wa Majengo mjini Moshi na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, CCM, wanachama wa UWT na wanawake wa mkoa huo.

Ndugai alisema  Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, na kwamba miongoni mwa mambo ambayo ametekeleza Rais ni kurejesha nidhamu kwa watumishi.

Alisema lingine ni kushughulikia tatizo sugu la rushwa ndani ya serikali, na ndani ya CCM hali ambayo itapunguza kwa kiasi kikubwa rushwa ya uchaguzi katika chaguzi zijazo.

“Serikali pia imepambana na mafisadi na kuanzisha mahakama ya mafisadi na pia amepunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kusitisha safari za nje zisizokuwa na Tija,” alisema.

Alisema jambo jingine ni kusimamia taratibu za makusanyo serikalini na kuongeza pato la taifa kutoka asilimia 5.1 hadi kufikia asilimia 7.5, kuongeza kasi ya ujenzi wa Miundombinu, kufufua shirika la ndege na kusimamia vyema rasilimali za nchi.

“Serikali imeendelea na mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu,kuimarisha miundombinu ya Maji na kuwa mtetezi wa wananchi walioonewa hasa wanawake,” alisema

Alitaja jambo la 11 ni kuteua tume ya uhakiki wa mali za chama , kufanya mageuzi makubwa ili kuhakikisha kilimo kinawanufaisha wakulima, kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara ili kuondoa ushuru wenye kero pamoja na bajeti ya serikali kugusa maisha ya wananchi.

Akizungumza mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudensia Kabaka, alisema kongamano hilo lililenga kumpongeza Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne na kwamba mambo makubwa yamefanyika katika kipindi hicho.

Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na naibu mawaziri watatu, wakuu wa taasisi za umma na mashirika ya umma ambao walipata fursa ya kueleza mafanikio ya Serikali.