Ndugai awa wa kwanza kuchukua fomu ya uspika

Spika wa Bunge anayemaliza muda wake, Job Ndugai amechukua fomu kwa ajili ya kutetea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili

Muktasari:

Baada ya dirisha la wagombea uspika kufunguliwa na CCM, Job Ndugai, spika anayemaliza muda wake amekuwa wa kwanza kuchukua na kurejesha fomu leo.

Dodoma. Spika wa Bunge anayemaliza muda wake, Job Ndugai amechukua fomu kwa ajili ya kutetea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

Ndugai ambaye amekuwa katika nafasi hiyo katika Bunge la kumi na moja amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na kuirejesha leo katika ofisi makao makuu ya CCM jijini hapa.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu kwa Katibu msaidizi idara ya oganaizesheni CCM Taifa, Solomon Itunda, Ndugai amewaomba Watanzania wamuombee ili chama kimteue katika nafasi hiyo.

"Ni utaratibu wa chama chetu wa kidemokrasia kuruhusu wanachama wenye sifa kugombea nafasi ya Spika na Naibu Spika kisha kufanya uteuzi. Niwaombe Watanzania waniombee ili niteuliwe na niwaambie kuwa wakati ukifika tutaongea nao," amesema Ndugai.

Akizungumza baada ya kupokea fomu ya Ndugai, Itunda amesema Ndugai amekuwa wa kwanza kuchukua na kurejesha fomu hizo.

Amesema yupo mwananchama mwingine ambaye alifika asubuhi kuchukua fomu lakini baadhi ya taarifa zake hazikukamilika ameondoka kuzikamilisha.

Itunda amesema fomu ya Spika na Naibu Spika kila moja inatolewa kwa gharama ya Sh500,000.

"Niwatake wanaCCM ambao wana sifa za kugombea nafasi wajitokeza kuchukua fomu. Zipo sifa mbalimbali ambazo zinatakiwa ikiwamo, kuwa mwananchama hai wa chama chetu na ni lazima awe raia wa Tanzania," amesema Itunda.

CCM ilifungua dirisha la kuchukua na kurejesha fomu hizo Novemba 2 hadi 3, 2020.