Ni Majaliwa tena?

Muktasari:

Kwa kuangalia mwenendo, historia, tabia ya marais waliopita na uteuzi ulioanza kufanyika, si vigumu kukuna kichwa kujiuliza kama Kassim Majaliwa atarejeshwa katika nafasi ya Waziri Mkuu.

Dar es Salaam. Kwa kuangalia mwenendo, historia, tabia ya marais waliopita na uteuzi ulioanza kufanyika, si vigumu kukuna kichwa kujiuliza kama Kassim Majaliwa atarejeshwa katika nafasi ya Waziri Mkuu.

Lakini ukweli kwamba Katiba hailazimishi kuteua mtu yuleyule kuendelea na nafasi ya Waziri Mkuu, unampa Rais John Magufuli nafasi ya kuteua mtu mwingine kama hakuridhishwa na utendaji wa mbunge huyo wa Ruangwa.

Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, marais wawili walioanzia mwaka 1995 hawakubadili mawaziri wao wakuu kwa utashi; Benjamin Mkapa, aliyeongoza awamu ya tatu, alianza na kumaliza na Frederick Sumaye na Jakaya Kikwete, aliyeongoza awamu ya nne, aliendelea na Mizengo Pinda aliposhinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Lakini Kikwete alilazimika kuteua Waziri Mkuu mwingine mwaka 2008 baada ya aliyekuwepo, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na sakata la mkataba wa Richmond.

Dalili za kujirudia kwa hali hiyo zimeanza kuonekana baada ya Rais Magufuli na makamu wake, Samia Suluhu Hassan kukubaliana Profesa Kilangi Adelardus aendelee na nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pia Kamati Kuu ya CCM imepitisha majina ya Job Ndugai na Dk Tulia Ackson kuwania nafasi za Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo kuna uhakika wa kushinda katika Bunge ambalo zaidi ya asilimia 90 ni kutoka chama hicho.

Swali linalofuata ni kama Rais Magufuli, ambaye ni mthubutu na asiyetabirika, ataendeleza utamaduni huo katika nafasi ya Waziri Mkuu.

“Kama Rais Magufuli anataka kuendeleza utaratibu wake wa zamani, atamteua tena Majaliwa kwa sababu amekuwa akitekeleza yale anayotaka,” alisema Buberwa Kaiza, mchambuzi wa siasa.

“Lakini kama anataka kubadilisha utaratibu wa uongozi wake, atateua mwingine kwa kadiri anavyopenda.”

Buberwa alisema kubadilisha mtu kunaweza kusababishwa na aina ya mtu anayemtaka kutekeleza majukumu ya Serikali kwa njia tofauti.

“Akitaka mtu ambaye hataki kusikiliza watu atamteua huyo (wa aina hiyo) au akitaka mtu anayependa demokrasia na kushauriana na watu kabla ya kuchukua uamuzi, atamteua huyo (wa aina hiyo),” alisema Buberwa.

Kwa mujibu wa Katiba, Rais anatakiwa kuwa ameteua mtu wa kushika nafasi hiyo muhimu ndani ya siku 14 baada ya kushika madaraka yake.

“Mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya siku 14, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni,” inasema ibara ya 51(2).

“Au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wabunge walio wengi.”

Na hiyo itafanyika baada ya Bunge la kwanza baada ya uchaguzi kuitishwa, kuchagua viongozi wake na baadaye Rais kuwasilisha jina la mtu anayempendekeza kuwa Waziri Mkuu ili aidhinishwe na wabunge.

Pamoja na watu kadhaa kuingia bungeni na baadhi kwa maombi makubwa ya Rais Magufuli katika kampeni zake, hakuna jina linaloibuka kuwa linaweza kurithi nafasi ya Majaliwa.

Majaliwa aliteuliwa Novemba 19, 2015 lakini uteuzi huo ulikosolewa kwa hoja kuwa mbunge huyo hakuwa na uzoefu baada ya kuingia bungeni mwaka 2010 na baadaye kushika nafasi ya naibu waziri wa Tamisemi kwa miaka mitano.

Lakini utu, ukweli, uadilifu, uzoefu wake kama mwalimu na kiongozi wa vyama vya wafanyakazi, ulimuwezesha kuonyesha wakosoaji kuwa alikuwa mtu sahihi kushika wadhifa huo.

Amekuwa mstari wa mbele na mtekelezaji mkubwa wa maagizo ya Rais na Serikali, akizunguka mikoani na kuanika uozo katika ngazi ya kuanzia wilaya hadi mkoa.

Majaliwa, ambaye alizaliwa Desemba 22, 1961 alisema Shule ya Sekondari ya Kigonsera. Alipata diploma ya ualimu Chuo cha Ualimu Mtwara alikomaliza mwaka 1993 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikomaliza mwaka 1998.

Baadaye alikuwa katibu wa wilaya wa Chama cha Walimu kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Urambo mwaka 2006. Mwaka 2010 aligombea ubunge wa Ruangwa na kushinda.

Juzi akitambua uwepo wa wageni mashuhuri, Rais Magufuli alishtua wasikilizaji alipomtaja Majaliwa kama “waziri mkuu mstaafu”, lakini akapoza mstuko huo kwa kicheko na kuendelea na hotuba yake fupi.

Mstaafu ni mfanyakazi aliyemaliza muda wake na ambaye anaweza kurudishwa kazini kwa mkataba maalumu, lakini neno hilo limekuwa likitumika kwa watu ambao hawako madarakani kwa sababu tofauti.

Uwezekano wa Majaliwa kuendelea na wadhifa wake ni mkubwa kulingana na hotuba za Rais Magufuli, ambaye aliwahi kudokeza kuwa alifanya kazi kubwa kupata jina lake miongoni mwa wengi.

“Wapo waliokuwa mawaziri, waliokuwa naibu mawaziri, waliokuwapo, wapo waliokuwa wabunge. Kwa hiyo nilikuwa na mtihani mkubwa na mtihani huo ilibidi nimuombe sana Mwenyezi Mungu anisaidie,” alisema Magufuli alipohutubia wananchi wa Ruangwa Oktoba 15, 2019.

“Siku ya mwisho ya kutangaza jina, na ninakumbuka sikulala vizuri. Jina lililokuwa likinijia lilikuwa ni la Majaliwa, Majaliwa tu. Sikuwa nimemweleza na ndiyo maana lilipotamkwa jina lake bungeni alianza kulia. Kwa sababu hata yeye hakutegemea kuwa waziri mkuu,” alisema Magufuli.

Alisema katika ziara hiyo alikwenda kumshukuru Majaliwa kwa kufanya naye kazi vizuri.

“Hata kufanya kazi na mimi ni kazi ngumu, lazima ujipange sawasawa, na hili nawaeleza ukweli kwa sababu na mimi ni mgumu. Hili Majaliwa ameliweza,” alisema Rais Magufuli.

Hata wakati akieleza sababu ya kuwaengua mawaziri Dk Charles Tizeba (Wizara ya Kilimo) na Charles Mwijage (Viwanda), Rais Magufuli alisema walishindwa kutimiza majukumu yao kiasi cha Majaliwa kuyabeba.

Majaliwa pia alipita bila kupingwa katika jimbo la Ruangwa na hivyo kupata nafasi kubwa ya kuzunguka mikoani kumpigia kampeni Magufuli, akitambulishwa kama “mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM”.

Suala hilo lilisababisha mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu kuhoji sababu za Majaliwa kuzunguka kufanya kampeni wakati hagombei urais.