Ni bunge la kuomba msamaha, je nani atafuata?

Mbunge wa Kigoma Kaskazini Peter Selukamba (CCM)

Muktasari:

Wabunge wameendelea kumiminika katika kuomba msamaha kwa viongozi wa CCM kuhusu kauli wanazotoa lakini Selukamba ametoboa kosa lake hadharani

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini Peter Selukamba (CCM) ameomba radhi bungeni kutokana na kauli aliyoitoa Juni mwaka huu katika mchango wake kuhusu kubeza ujamaa kwamba hakuwa na maana hiyo.

Selukamba ametumia kanuni ya 50 ya Bunge leo Septemba 12,2019  na kueleza kuwa alinukuliwa vibaya hata kusababisha usumbufu kwa chama chake na viongozi wake.

Huyu anakuwa mbunge wa kwanza kueleza hadharani kosa lililofanya aombe msamaha wakati wengine wamekuwa hawatajwi makosa yao hadharani.

Spika Job Ndugai alimuita Selukamba kuwa anampa muda mchache kueleza jambo lililombele yake ndipo mbunge huyo  akasimama.

"Juni wakati nahitimisha hoja yangu hapa bungeni nlitumia neno ujamaa vibaya kwa kusema kuwa kama kuna jambo siliamini ni ujamaa,"amesema Selukamba.

"Naomba radhi chama changu naomba radhi kwa viongozi wangu kwa usumbufu wowote walioupa kuhusu kauli yangu, sikuwa na maana kama ilivyochukuliwa."

Selukamba amesema yeye ni zao la CCM, chama ambacho kinaamini katika ujamaa na hivyo na yeye ni mjamaa kama ilivyo kwa chama chake.

Mbunge huyo ameomba radhi ikiwa ni muda mfupi baada ya Spika Ndugai kutangaza bungeni kwa kuwashukuru wabunge Nape Nnauye,William Ngeleja na January Makamba kwamba walifanya jambo lenye maana kubwa kwa kumuomba radhi