Nimr yazungumzia saratani kanda ya Ziwa

Muktasari:

  • Julai 15 mwaka 2019, Rais wa Tanzania, John Magufuli aliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa saratani katika mikoa ya kanda ya ziwa ambayo alidai wagonjwa wengi wanatoka mikoa hiyo.

Dodoma. Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) nchini Tanzania imesema hakuna takwimu za kuthibitisha kuwa mikoa ya kanda ya Ziwa inaongoza kuwa na wagonjwa wa saratani.

Kauli hiyo imetolewa jana Jumatatu Januari 20,2020 na Mkurugenzi Mkuu wa Nimr, Profesa Yunus Mgaya mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilipokuwa ikitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake.

Profesa Mgaya alisema taasisi yake ilifanya utafiti ambao ulihusisha takwimu za miaka mitano (2015 hadi 2019) kutoka katika Hospitali za Bugando jijini Mwanza na Ocean Road, Dar es Salaam.

Alisema takwimu za wagonjwa wa saratani zilizohusishwa katika utafiti huo ni wagonjwa 16,546 kutoka hospitali ya  Ocean Road na 4,562 kutoka Bugando.

Alisema utafiti huo wa awali ulilenga katika kujua ukubwa wa tatizo la saratani nchini.

Alisema utafiti utakaofuata utakuwa wa kina ambao utaangalia watu walipo, visababishi ambapo watangalia  mazingira, shughuli wanazofanya, uchafuzi wa hewa,  wanaoishi na vyakula wanavyokula.