Makonda: Nitawatetea wanawake Dar hata nikichukiwa na wanaume

Sunday September 08 2019
makonda1 pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema yupo tayari kuchukiwa na wanaume wa Mkoa huo wanaokwazika na uamuzi wake wa kuwatetea wanawake.

Amesema hawezi kukaa kimya kuangalia mateso ya wanawake yanayoweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa wanaume watabadilika.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumapili Septemba 8, 2019 katika Kanisa la Inuka Uangaze la Mtume  Boniface Mwamposa  maarufu 'Bulldozer' lililopo Kawe, Dar es Salaam.

Amesema wakati wa wanawake kutembea kifua mbele umefika na siku zote atasimama kuwatetea.

“Wanawake wakati wa kutembea kifua mbele umefika, kama mlimbeba mtoto miezi tisa hakuna jambo litakalokushinda. Wanaume mjipange, siwezi kukaa kimya kwa ajili ya mama,” amesema Makonda.

Amesema baada ya kuwasilisha serikalini mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya ndoa, anajipanga pia kupeleka mabadiliko ya sheria ya mtoto.

Advertisement

“Katika sheria ya mtoto tumependekeza matunzo yaanzie mimba inapoingia, mtoto atunzwe kuanzia hapo. Wasichana wengi wanatelekezwa wakipata ujauzito kwa madai mimba imeingia kwa bahati mbaya.”

“Wasichana wa kazi wanateseka, wanapewa mimba na mabosi zao na kufukuzwa wakiambiwa wataharibu ndoa. Kama unajijua una ndoa jisitiri na ndoa yako unahangaika ili iweje. Hadi niondoke kwenye huu mkoa kuna watu mtakuwa mmenyooka,” amesema Makonda.

Advertisement