Nundu: Bila Magufuli TTCL ingekufa

Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL),  Omari Nundu

Muktasari:

Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL),  Omari Nundu amesema kama siyo upendo wa Rais John Magufuli shirika hilo lingekufa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL),  Omari Nundu amesema kama siyo upendo wa Rais John Magufuli shirika hilo lingekufa.

Nundu ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 21, 2019 katika hafla ya shirika hilo kutoa gawio kwa Serikali iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma ya video conference.

“Tuna kazi kubwa kumuelimisha Mtanzania ajue hivyo na awe na shauku ya kuliunga mkono na kutumia huduma zake, jitihada tunazifanya,” amesema Nundu.

Amesema kitendo cha Rais Magufuli kwenda kupokea gawio makao makuu ya ofisi za shirika hilo kumewapa ari ya kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanatengeneza faida ya kutosha.

“Tukio la leo linaendelea kuandika historia chanya ya taasisi hii ambayo imepita katika misukosuko mingi. Ninawashukuru  watumishi wote wanavyoendelea kurejesha uimara wa shirika katika kipindi kifupi cha utawala wako,” amesema Nundu.

Amebainisha kuwa gawio lililotolewa leo  limetokana na faida ya Sh8.3 bilioni iliyopatikana, kwamba mwaka 2019 mapato ya jumla yalikuwa Sh119 bilioni huku matumizi yakiwa Sh111 bilioni.