Nyalandu ashinda uchaguzi Chadema

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini nchini Tanzania,  Lazaro Nyalandu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati baada ya kupata kura 60 kati ya 86 zilizopigwa.

Dodoma. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini nchini Tanzania,  Lazaro Nyalandu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati baada ya kupata kura 60 kati ya 86 zilizopigwa.

Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii ameshinda kwa asilimia 66.8 katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma na kusimamiwa na mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Sosopi akisaidiana na katibu mkuu wa baraza hilo, Julius Mwita.

Akitangaza matokeo hayo leo Jumapili Desemba Mosi, 2019, Sosopi amesema waliopiga kura walikuwa 86, hakuna kura iliyoharibika.

Amesema aliyekuwa mwenyekiti wa Kanda hiyo, Alphonce Mbasa amepata kura 26, sawa na asilimia 33.2.

Katika nafasi ya mweka hazina, Mbunge wa Viti Maalum,  Devotha Minja ameibuka mshindi baada ya kupata kura 44 sawa na asilimia 51.2 huku mshindani wake, Tully Kiwanga akipata kura 42 sawa na asilimia 48.8.

Uchaguzi wa makamu mwenyekiti  umerudiwa baada ya kukosekana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50.