Nyaraka zazua mjadala kesi ya kina Kitilya

Dar es Salaam. Mawakili wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mwenyekiti wa kampuni ya uwekezaji wa mitaji na dhamana ya Egma, Harry Kitilya na wenzake wanne, wameiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi, kulitupa ombi la upande wa utetezi la kupinga kupokewa nyaraka wanazotaka zitumike kama vielelezo.

Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya Jaji Emmaculata Banzi baada ya shahidi wa saba wa upande wa mashtaka, ambaye ni mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Devotha Makani (awali alikuwa Wizara ya Fedha) kuomba kutoa nyaraka zilizoombwa na Takukuru na akaziwasilisha. Kati ya nyaraka zilizowasilishwa Takukuru na Makani ni muhtasari wa kikao cha kamati ya ufundi ya kusimamia madeni (TDMC) na muhtasari wa kikao cha kamati ya Taifa ya kushughulikia madeni (NDMC).

SOMA ZAIDI: KESI YA KINA KITILYA: Serikali ilivyoweka msingi wa kesi katika kikao cha kwanza kuelekea cha pili

Nyaraka nyingine ni faili, dokezo sabiri (loosing document), ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwenda kwa Waziri wa Fedha na maombi ya ushauri huo kutoka kwa Waziri wa Fedha kwenda kwa AG.

Baada ya Makani akiongozwa na wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya kuwasilisha ombi hilo, mawakili wa utetezi walipinga. Alianza Masumbuko Lamwai aliyeiomba mahakama isipokee nyaraka hizo kwa kuwa haziendani na kielelezo namba 28 ambacho ni barua iliyoandikwa na Makani wakati akiwasilisha nyaraka hizo Takukuru.

Makani alisema barua hiyo ilikuwa na vipengele vinne kikiwamo kinachohusu faili ambalo kwa mujibu wa Lamwai halipo mahakamani na kila muhtasari ndani ya faili hilo aliipa namba.

Lamwai alisema nyaraka zilizowasilishwa hazina hizo folio namba hivyo zimetengenezwa.

Aliiomba mahakama isipokee nyaraka hizo kwa sababu ushahidi wa shahidi huyo haujakidhi matakwa ya sheria.

Naye wakili Majura Magafu alisema kifungu cha 103 cha sheria ya ushahidi kinataka nyaraka zizungumze zenyewe. Kwa kuangalia kielelezo cha barua ya Januari 4, 2016 iliyoandikwa na Makani kwenda Takukuru inasema nyaraka zina folio namba, lakini zilizopo mahakamani hakuna hata moja inayoonyesha hilo. Pia, alisema upande wa mashtaka ulishindwa kumjengea msingi shahidi kueleza yalipo mafaili wanayozungumzia hilo.

Wakili Alex Mgongolwa alisema faili namba zipo ili kueleza matukio na si urembo, hivyo akaomba nyaraka zisikubalike kwa kuwa zina mapungufu.

Wakili Charles Anindo naye alisema kuna uwezekano mkubwa nyaraka zilizowasilishwa Takukuru sio zilizopelekwa mahakamani hapo kwa kuwa zilizopelekwa Takukuru shahidi anaeleza alizipa folio namba.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali, Awamu Mbagwa aliiomba mahakama isikubaliane na mapingamizi yote kwa sababu hayana mashiko na ipokee yaraka hizo. Alisema shahidi huyo ana uhalali wa kutoa nyaraka hizo na hakuna tofauti yoyote kati barua ya Januari 4, 2016 na ushahidi wa shahidi huyo hoja iliyojibiwa na Magafu aliyesema kuwa ni ya msingi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Banzi aliiahirisha kesi hiyo hadi leo saa 8:00 mchana atakapotoa uamuzi kuhusu nyaraka hizo.

Wengine katika kesi hiyo ni Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana wanaokabiliwa na mashitaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya dola 6 milioni za Kimarekani, kujipatia fedha hizo kwa udanganyifu na utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Shahidi huyo mkurugenzi wa rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha na katika ushahidi wake alidai miongoni mwa majukumu yake yalikuwa ni kusimamia masijala ya wizara hiyo, ya siri na kutunza nyaraka za Wizara ya Fedha.