Nyerere, Karume wasaini hati za Muungano - 12

Rais wa Tanganyika Mwalimu Nyerere(kushoto) akikabadilishana hati za makubaliano ya Muungano na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume . Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere alivyotua Zanzibar kwa ziara ya saa chache ya kirafiki, wakati vuguvugu la Muungano likiendelea huku mabalozi wa Marekani wa Tanganyika na Zanzibar wakifuatilia kwa makini na kutuma taarifa ya kila kinachoendelea.Endelea…

Jana tuliona jinsi Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere alivyotua Zanzibar kwa ziara ya saa chache ya kirafiki, wakati vuguvugu la Muungano likiendelea huku mabalozi wa Marekani wa Tanganyika na Zanzibar wakifuatilia kwa makini na kutuma taarifa ya kila kinachoendelea.

Endelea…

Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere aliwasili Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kwa ndege ya Tanganyika akiongozana na waziri mdogo katika Ofisi ya Rais, Bhoke Munanka.

Nyerere alilakiwa na mwenyeji wake, Sheikh Abeid Amani Karume Makamu wa Rais wa Zanzibar, Sheikh Kassim Hanga; Waziri wa Fedha, Abdul Aziz Twala; Katibu wa Bunge na Baraza la Mapinduzi; Salim Rashid pamoja na wanachama wengine wa SMZ.

Watanganyika waliotangulia Zanzibar siku hiyo asubuhi ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ulinzi, Oscar Kambona na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Lusinde.

Baada ya kulakiwa, Karume na Nyerere walienda Ikulu ya Zanzibar na kufanya mazungumzo ya siri, wakiwaacha mawaziri wao nje wakiwa kwenye veranda.

Mazungumzo yao yalidumu kwa muda wa nusu saa tu. Walipotoka walionekana wamefurahi kisha wakasaini kile kilichoitwa hati za mkataba wa Muungano.

Akizungumza kuhusu ziara ya Nyerere, Katibu wa Bunge la Mapinduzi, Salim Rashid anadaiwa kuwanong’oneza Kambona na Lusinde na kusema “mnakaribishwa sana Zanzibar”.

“Bila shaka,” akasema Kambona, kisha akatabasamu wakati wakipeana mikono ya maagano. Lakini Lusinde hakuwa mzungumzaji sana, kana kwamba hakuamini yaliyokuwa yakitokea.

Kabla Nyerere hajaondoka, Salim Rashid akawaambia waandishi wa habari kuhusu mkutano huo.

“Watu wa nchi zetu mbili wamekuwa marafiki siku zote kiasi cha kuwa jambo la asili kwa viongozi wetu kukutana mara kwa mara kuzungumza matatizo yanayotuhusu,” alisema.

Alipomaliza mazungumzo na Rais Karume saa 8:20 mchana, Mwalimu Nyerere alipanda ndege na kurejea Dar es Salaam. Alitumia dakika 100 tu kuingia na kuondoka Zanzibar.

Akiagana na akina Salim Rashid, Kambona alisema: “Siku za usoni, Rais Nyerere atatembelea tena Zanzibar.” Kisha waliongozana na Job Lusinde na kuingia katika ndege iliyowarejesha Dar es Salaam dakika chache baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka.

Siku hiyo usiku ndipo lilipotolewa tangazo hadharani kwamba “Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Unguja, Sheikh Abeid Aman Karume, wametia saini hati za makubaliano kati ya Tanganyika na Zanzibar”.

Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC) lilifanya kazi ya kuwaeleza Watanganyika kile ambacho viongozi wao walitaka wakijue.

Jioni ya siku hiyo saa 2:00 usiku, wakati tangazo la kuziunganisha nchi likitolewa jijini Dar es Salaam, Oscar Kambona alitua mjini Nairobi, Kenya kwa ajili ya “mazungumzo muhimu” na Waziri Mkuu (mpaka wakati huo) wa Kenya, Jomo Kenyatta. Safari hiyo haikuripotiwa.

Alikutana na Kenyatta katika nyumba yake iliyoko Gatundu na pamoja naye alikuwepo Henri Warith, ambaye alikuwa katibu wa Bunge.

Alimwelewesha kuhusu mapatano ya Tanganyika na Zanzibar kuunda serikali moja.

Kama alifurahi au la, Warith alionekana kushangazwa na kilichokuwa kikizungumzwa.

“Ahaa! Kwa hiyo huu ndio mwanzo wa shirikisho?” alihoji.

Alikuwa mmoja wa watu waliohudhuria mkutano wa wakuu watatu kuhusu shirikisho la nchi za Afrika Mashariki ambao ulivunjika Aprili 11, 1964 bila maafikiano.

Baadaye Kambona akaenda Kampala kukutana na Waziri Mkuu wa Uganda, Dk Milton Apollo Obote kwa sababu hizo hizo.

Itaendelea kesho