MIAKA 20 BILA NYERERE: Nyerere apata msukosuko-5

Muktasari:

Usiku wa Jumamosi ya Januari 18 kuamkia Jumapili ya Januari 19, 1964 kulitokea maasi ya kijeshi katika mji wa Dar es Salaam yaliyoanzia kwenye Kambi ya Colito (sasa Lugalo) ya Jeshi la King African Rifles (KAR). Kilichosababisha kile kilichoitwa ‘Maasi ya Dar es Salaam’ bado kinabaki kama fumbo. Ingawa kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa harakati za kisiasa za Watanganyika zilianza mwaka 1929 kwa kuanzishwa kwa Chama cha Tanganyika African Association, hakuna wakati mwingine wowote ambao Tanganyika ilikuwa imeingia majaribuni kama Januari 1964.

Nia yake (Nyerere) iliyojaa busara ya kuendelea kulijenga taifa inaonekana inaanza kueleweka kwa watu wake (Watanganyika), hususan katika kauli mbiu yake, Uhuru ni Kazi. Lakini ghafla jambo fulani lisilotarajiwa linatokea katikati ya nia yake.

Jeshi la King African Rifles (KAR) linaasi; ghasia zinazuka katika mitaa ya Dar es Salaam. Watu wanauawa. Mali zinaporwa. Alinusurika tu kwa kuita majeshi ya Uingereza. Wakati moto ulipotulia, swali la kutisha likakosa jawabu: Ikiwa Nyerere anaweza kutikiswa hata kufikishwa kwenye ukingo wa kuangamia, ni nani aliye salama katika Bara la Afrika?

Hayo yaliandikwa na jarida la TIME la Marekani (Machi 13, 1964), ikiwa ni siku 53 tu tangu kulipotokea maasi ya kijeshi katika Tanganyika. Je, jarida hilo liliona kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa salama kuliko kiongozi mwingine yeyote Afrika kiasi cha kuuliza swali hilo la kutisha?

Kuna siku ambazo historia rasmi ya Tanzania haipendi kuzikumbuka, lakini haitaweza kuzisahau. Januari 19, 1964, siku kulipotokea maasi ya KAR, ni miongoni mwa siku hizo. Hiyo ilikuwa ni wiki moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12.

Hata Mwalimu Nyerere alijua kuwa ni vigumu kusahau. Kwa huzuni Nyerere alikaririwa na jarida la TIME (Jan. 31, 1964), chini ya makala yake, ‘The Rise of the Rifles,’ akisema: “Itachukua miezi na hata miaka, kufuta katika bongo za walimwengu kile walichosikia kuhusu matukio ya juma hili.” Hata hivyo imeshaanza kufutika katika bongo za walimwengu.

Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 18-19, 1964 kulitokea zahama mjini Dar es Salaam katika kambi ya Jeshi la KAR ya Colito (sasa Lugalo), ambalo ilisambaa hadi kambi nyingine nchini.

Baada ya tukio hilo, maswali mengi yaliulizwa. Ingawa tayari mengi yamejibiwa, mengi hayajatosheleza. Je, yalikuwa mapinduzi ya serikali (kama yale ya Zanzibar)? Yalikuwa ni maasi tu ya KAR? Ulikuwa ni mgomo tu wa wanajeshi waliotaka kuongezwa mishahara?

Majibu yaliyotolewa na wale walioitwa—au waliojiita—wanasayansi wa siasa yalijaribu kupunguza uzito wa maasi hayo kutoka katika mapinduzi ya serikali na kuyafanya yaonekana kana kwamba yalikuwa ni mgomo tu wa wanajeshi wa KAR kutaka kuongezwa mishahara na vyeo.

Tafsiri zao zilikuwa hivi: kama ingekuwa ni mapinduzi, ilikuwa ni lazima kwanza wanajeshi walioasi wangeteka maeneo yote muhimu ya kama Bunge na Ikulu. Ilikuwa ni lazima wawakamate mawaziri, jambo ambalo hawakufanya. Hawakuwa wamemtangaza kiongozi wa nchi.

Huenda haikuwa mapinduzi ya serikali, lakini kwa namna fulani ilikuwa ni mapinduzi ya aina yake. Ilidaiwa kuwa aliyekuwa afaidike na maasi hayo ni waziri wa zamani wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Tanganyika, Oscar Kambona ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Kassim Hanga wa Zanzibar.

Kwa kawaida Kambona alijua au alikuwa amearifiwa mapema kuhusu maasi ya Dar es Salaam katika vitengo vya usalama vya Tanganyika na maofisa wa Kiingereza ambao bado walikuwa wakiitumikia Serikali ya Tanganyika, lakini hakuchukua hatua yoyote kuikabili hali hiyo hadi pale ilipotokea. Mmoja wa maofisa hao ni Luteni Kanali Rowland Mans.

Ilidaiwa kuwa mara kwa mara, Kambona, akiwa Waziri wa Ulinzi, alikuwa akiwatembelea maofisa wa KAR ngazi za chini katika kambi ya Colito, na mara nyingine bila kuonana na viongozi wakubwa wa kambi hiyo.

Pia, kwa sababu zisizojulikana dhahiri lakini ambazo inawezekana ni njia ya kumsaidia Kassim Hanga, Kambona alitenga silaha na zana nyingine za vita zilizotoka Algeria na kuwasili Dar es Salaam Jumatano ya Januari 3, 1964 na kupakuliwa chini ya ulinzi maalum.

Silaha hizo ziliwasili siku tisa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar na wiki mbili kabla ya maasi ya Dar es Salaam.

Silaha hizi, baada ya maasi ya Dar es Salaam, inadaiwa—na hii inadaiwa tu zilichukuliwa na kutoswa baharini na Jeshi la Maji la Uingereza lililoombwa na Serikali ya Tanganyika Jumamosi ya Januari 25, 1964, kukomesha maasi ya jeshi Dar es Salaam.

Hata hivyo nyingi za silaha hizo zilitumiwa wakati wa Vita Kuu II Kaskazini mwa Afrika. Zilitumiwa na Waingereza, Wajerumani na Waitaliano na zingekuwa vigumu kutumiwa miaka ya 1960 kwa kuwa hazikuwa na vipuri.

Inasemekana kwamba silaha hizo ziliagizwa na Serikali ya Tanganyika kwa ajili ya chama cha Frelimo cha Msumbiji. Zilipowasili Dar es Salaam, pamoja na kwamba maofisa wakubwa wa Jeshi la Tanganyika walikuwa ni Waingereza, silaha hizo zilipakuliwa na wanajeshi Waafrika tu.

Inasemwa pia kwamba silaha hizo hazikuhifadhiwa kama ilivyopaswa, kwa hiyo zikawafanya Waingereza washtuke. Walipozichunguza sana wakagundua kuwa zana nyingine zilitiwa alama ya msalaba mweusi, wakachukulia hizo zilizotiwa alama zilikusudiwa kupelekwa Zanzibar kumsaidia Kassim Hanga kulingana na tetesi walizokuwa wamezipata hapo awali. Lakini silaha hizo hazikuwahi kufika Zanzibar. Je, zilikusudiwa kutumika wakati wa maasi ya KAR yaliyotokea Dar es Salaam?

Kwa mujibu wa utafiti wa Nestor Luanda katika kitabu ‘Tanganyika Mutiny’, Kambona alianza kufika mara kwa mara katika Makao Makuu ya Jeshi mwishoni mwa 1963 na aliwaambia maofisa wa kijeshi wa Kiingereza kwamba alitaka wawe wameondoka nchini ifikapo mwishoni mwa 1964.

Kambona alitaka maofisa wengi wa Kitanganyika wapewe vyeo haraka, jambo ambalo Waingereza walidai haliwezi kutendeka kwa ghafla kama alivyotaka. Kuanzia hapo maofisa hao wakaanza kuwa na wasiwasi kuwa chochote kinaweza kutokea.

Ingawa uhusiano wa maofisa wa kijeshi wa Uingereza na Waziri Kambona ulianza kupungua, huo si ushahidi wa kutosha kueleza kuwa Kambona alihusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Hata hivyo, usiku ule wa maasi maofisa wengi wa Kiingereza walikamatwa na kutiwa ndani katika Kambi ya Colito ambako kwa wakati huo umeme tayari ulikuwa umekatwa.

Kikosi cha kiasi cha wanajeshi 25 wa KAR waliondoka kambini hapo kwenda Ikulu kumfuata Rais Julius Nyerere kikiongozwa na mwanajeshi machachari, Sajenti Francis Hingo Ilogi, mzaliwa wa Bukene, Tabora.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Emilio Mzena, baada ya kuambiwa yaliyotokea na kwamba wanajeshi wa KAR walio na silaha wameelekea Ikulu, aliwaarifu watu wake waliokuwa Ikulu na kuwaambia wamtoroshe Rais.

Mzena aliambiwa kuhusu maasi hayo majira ya saa 8:00 usiku. Nusu saa baadaye, saa 8:30, baada ya kuamshwa na walinzi wao, Rais Nyerere, akiongozana na Makamu wake, Rashidi Kawawa, waliondoka Ikulu kupitia mlango wa nyuma. Walipishana na wanajeshi hao kwa sekunde chache tu.

Baadaye wanajeshi hao wa KAR walipelekwa kwa Kambona, wakamchukua kwenda naye kambini kwao, Colito. Wakati huo ghasia na uporaji mali za raia tayari ulikuwa umetanda katika mitaa ya mji wa Dar es Salaam.

Wakati hayo yakitokea, tayari wanajeshi hao wa KAR walianza kupeana vyeo huko huko kambini. Wengine walipokea vyeo hivyo lakini wengine hawakuharakisha kupokea. Kwa mfano, Sajini Francis Hingo Ilogi anayedaiwa kuongoza maasi hayo, alikuwa na cheo cha Sajini lakini alijikuta katika cheo cha Luteni Kanali na wengine walimtaka mtu kama Kapteni Alex Nyirenda kuwa Brigedia.

Itaendelea kesho...