MIAKA 20 BILA NYERERE: Nyerere ateua baraza la kwanza la mawaziri-4

Muktasari:

Katika chaguzi za wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (Legco) zilizofanyika mwaka 1958, 1959 na 1960, chama cha Tanu kiliibuka na ushindi. Baada ya ushindi wa mwaka 1958 na 1959, kulikuwa na matumaini ya kupatikana uhuru wa Tanganyika...

Baada ya Tanu kupata tena viti vingi katika uchaguzi wa 1960, Gavana Richard Turnbull alimwambia Mwalimu Nyerere aunde serikali. Mkutano wa Katiba ulifanyika mjini London, Machi 1961.

Hatimaye Tanganyika ikapata serikali ya kujitawala Jumatatu ya Mei 1, 1961 ingawa bado gavana alikuwa na mamlaka fulani katika mambo muhimu ya nchi. Hata hivyo Nyerere akawa waziri mkuu wa kwanza na baraza lake la mawaziri likawa kama ifuatavyo:

Rashidi Mfaume Kawawa:

Aliteuliwa waziri asiye na wizara maalumu kabla hajawa Waziri wa Serikali za Mitaa. Baada ya Nyerere kujiuzulu uwaziri mkuu, 1962, alimteua Kawawa kuwa waziri mkuu na kudumu na wadhifa huo hadi Desemba 9, 1962 Tanganyika ilipokuwa Jamhuri. Agosti 1958 alichaguliwa kuingia Baraza la Kutunga Sheria na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Nyumba. Alizaliwa Songea Alhamisi ya Mei 27, 1926. Alifariki Desemba 31, 2009 akiwa na miaka 83.

Abdallah Said Fundikira:

Aliteuliwa Waziri wa Ardhi, Upimaji Ramani na Maji. Huyu alikuwa Mtemi wa 19 wa Unyanyembe. Utawala wake ulidumu miaka mitano tu 1957-1962. Nyerere alifuta utemi wa dola rasmi mwaka 1962. Hata hivyo, baada ya utemi kufutwa, aliteuliwa kuwa waziri. Alizaliwa Februari 2, 1921 huko Unyanyembe. Alifariki Agosti 6, 2007, akiwa na miaka 86.

Sir Ernest Vasey:

Aliteuliwa Waziri wa Fedha, hakuwa Mtanganyika. Aliingia Afrika Mashariki mwaka 1936 na kukaa Kenya miaka 23 huku akishika nyadhifa mbalimbali ikiwamo mbunge wa kuchaguliwa wa Nairobi Kaskazini. Mwaka 1952 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Maendeleo wa Kenya hadi 1959. Alipoingia Tanganyika, Februari 1960, akateuliwa Waziri wa Fedha wa Tanganyika. Sir Vasey aliteuliwa na Gavana, kwa maombi ya Mwalimu Nyerere, kuingia Legico, kabla ya Nyerere kumteua kuwa waziri. Alisoma bajeti yake ya kwanza mwaka wa fedha wa 1960/61, Aprili 7. Nyerere alipojiuzulu uwaziri mkuu, Sir Vasey naye alijiuzulu nafasi yake. Alizaliwa 1901, Uingereza. Alifariki 1984 akiwa na miaka 83.

Amir Habib Jamal:

Alikuwa Waziri wa Viwanda. Ni Mhindi pekee aliyekuwa katika serikali ya kwanza ya Tanganyika na ambaye aliendelea kuwapo baada ya uhuru. Juni 1959 aliingia serikalini mara ya kwanza alipoteuliwa kuwa Waziri wa Tawala za Miji na Majengo katika serikali ya muda ya Tanganyika. Uteuzi huo ulitokana na uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958. Jamal, mwenye asili ya India, alizaliwa Januari 26, 1922 nchini Tanganyika na alifariki Machi 21, 1995 akiwa na miaka 73.

Asanterabi Zephaniah Nsilo Swai:

Aliteuliwa Waziri wa Biashara. Kabla ya hapo alikuwa meneja mkuu Chama cha Ushirika Meru na alikuwa mwenyekiti wa Tanu mkoa wa Kanda ya Kaskazini. Alikuwa pia mwenyekiti kamati ya uchumi na ustawi wa jamii ya Tanu. Alipata elimu vyuo vikuu vya Makerere, Uganda; Bombay, India na Pittsburg, Marekani na Chuo Kikuu cha Delhi, India. Alizaliwa Aprili 20, 1925 Moshi, Kilimanjaro na kufariki Januari Mosi, 1994 akiwa na miaka 69.

Tewa Said Tewa:

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Upimaji. Alizaliwa mwaka 1924 jijini Dar es Salaam, alikuwa akiishi Magomeni Mikumi na mmoja wa watu wa mwanzo kumpokea na kufahamiana na Nyerere alipokuja Dar es Salaam mwaka 1952. Tewa ni kati ya wale wazalendo 17 walioasisi Tanu. Alifariki mwaka 1998 akiwa na miaka 74.

Paul Lazaro Bomani:

Alikuwa Waziri wa Ukulima na Maendeleo ya Ushirika. Mzaliwa wa Ikizu, Musoma, aliingia katika serikali ya Nyerere akiwa na miaka 35. Kama Kahama. Bomani naye alijishughulisha sana na ushirika katika Kanda ya Ziwa na alikuwa kiongozi wa chama cha Ushirika cha Victoria Federation of Co-operative Unions (VFCU). Alipata elimu ya ushirika Chuo cha Loughborough, Uingereza. Mwaka 1958 alipita bila kupingwa kuwa mjumbe wa Legico. Alizaliwa Januari Mosi, 1925. Alifariki Aprili Mosi, 2005 akiwa na miaka 80.

Oscar Salathiel Kambona:

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa na miaka 32. Kambona, alikuwa mtoto wa kasisi na alipata elimu yake shule za Alliance zilizokuwa Dodoma na Tabora. Alisoma sheria Chuo Kikuu cha Middle Temple, London, Uingereza na wakati anateuliwa kuingia Baraza la Mawaziri alikuwa Katibu Mkuu wa Tanu. Alizaliwa Agosti 13, 1928, Kwambe karibu na Mbamba Bay. Alifariki mjini London Julai 1997 akiwa na miaka 69.

Derek Noel Maclean Bryceson:

Alikuwa mkulima, lakini aliteuliwa Waziri wa Afya na Masuala ya Wafanyakazi akiwa na miaka 37. Bryceson aliingia Tanganyika mara ya kwanza mwaka 1952 akitokea Kenya. Alisoma Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza na alikuwa katika kikosi cha Jeshi la Anga la Uingereza wakati wa Vita Kuu, II ya Dunia. Mara ya kwanza aliingia serikalini mwaka 1957 kwa cheo cha Waziri Msaidizi wa Kazi za Starehe, na baadaye, Juni 1959, akawa Waziri wa Machimbo ya Madini na Biashara, na mwaka uliofuata, 1960, akaingia katika Serikali ya Mwalimu Nyerere. Tofauti na Wazungu wenzake waliokuwa katika serikali ya Nyerere, Bryceson alikuwa mjumbe wa kuchaguliwa wa Legico wa Jimbo la Kaskazini. Bryceson ni raia wa Uingereza aliyezaliwa China, Desemba 31, 1922. Alifariki, Oktoba 1980 akiwa na miaka 58

Clement George Kahama:

Aliteuliwa kuwa Waziri wa Usalama na Amani ya Nchi (Waziri wa Mambo ya Ndani). Kahama kutoka Karagwe, aliteuliwa uwaziri akiwa na miaka 32. Alipata elimu Sekondari ya Tabora na Chuo cha Loughborough, Uingereza. Alikuwa mtunza hazina chama cha wakulima cha Bukoba (BCU) na kiongozi mkuu wa kwanza wa ushirika huo mwaka 1956. Alijishughulisha sana na halmashauri ya mji wa Bukoba na halmashauri ya Buhaya na aliingia Legico kutoka Jimbo la Ziwa Magharibi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1958. Alizaliwa Karagwe Novemba 30, 1929. Alifariki jijini Dar es Salaam, Machi 12, 2017 akiwa na miaka 88.

Job Malecela Lusinde:

Aliteuliwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Alijiunga na Tanu mwaka 1955 baada ya kurejea kutoka masomoni Makerere, Uganda. Katika Jimbo la Kati, Lusinde alikuwa naibu katibu wa Tanu wa jimbo. Mwaka 1959 alikuwa ofisa mtendaji halmashauri ya wilaya ya Dodoma kabla ya kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo mwaka 1960. Alizaliwa Oktoba 9, 1930 mkoani Dodoma.

Baada ya Tanganyika kuwa Jamhuri, Nyerere alifanya mabadiliko kidogo ya Baraza la Mawaziri. Alifuta cheo cha waziri mkuu na kuunda cha Makamu wa Rais kama Katiba ilivyotaka. Na Kawawa akawa Makamu wa Rais.

Katika mabadiliko hayo, Chifu Abdallah Fundikira aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria lakini alijiuzulu mwaka uliofuata yaani 1963, baada ya kutuhumiwa kwa rushwa.

Kambona alichukua uwaziri wa Mambo ya Ndani kutoka kwa George Kahama. Katika mabadiliko ya mwaka 1963, Kambona akawa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi. Kabla ya mwaka 1963 wizara hiyo ilikuwa chini ya Rais Nyerere. Kahama akawa Waziri wa Biashara. Bomani akachukua uwaziri wa Fedha kutoka kwa Ernest Vasey.

Nyerere akaongeza na mawaziri wengine. Hao ni pamoja na Sheikh Amri Abeid, Jeremiah Kasambala, Saidi Ali Maswanya, Michael Kamaliza, Austin Shaba, Lawi Nangwanda Sijaona na Solomon Eliufoo.

Kutokana na hilo, baraza jipya la mwaka 1963 likawa na Sheikh Amri Abeid (Waziri wa Sheria), Bryceson (Kilimo), Kahama (Biashara), Kambona (Mambo ya Nje na Ulinzi) na Lusinde (Mambo ya Ndani).

Wengine ni Jamal (Mawasiliano), Bomani (Fedha), Tewa (Ardhi), Kasambala (Ushirika na Maendeleo ya Jamii), Eliufoo (Elimu), Maswanya (Afya) na Kamaliza (Kazi).

Pia walikuwapo Shaba (Serikali za Mitaa), Sijaona (Mila na Utamaduni), Swai (Mipango ya Maendeleo). Nafasi ya uwaziri mkuu ilirejeshwa Februari 1972 alipoteuliwa Kawawa hadi mwaka 1977 alipoteuliwa Edward Moringe Sokoine.