Nyota wa zamani Chelsea kuinunua klabu ya Sampdoria

Thursday August 22 2019

 

By AFP

Turin, Italia. Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Italia na klabu ya Chelsea, Gianluca Vialli anaongoza kundi la wawekezaji ambalo linakaribia kuinunua klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya soka ya Serie A, Sampdoria, kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa leo Alhamisi.
Kundi la mmiliki wa Sampdoria, Massimo Ferrero limesaini barua ya nia ya kampuni ya Vialli kufanya mazungumzo peke hadi Septemba kwa ajili ya kubadilisha umiliki wa klabu hiyo, vyombo vya habari vya Sky Sport Italia na Gazzetta Dello Sport vimeripoti leo Alhamisi.
Kundi hilo linaloitwa CalcioInvest consortium la Vialli, pamoja na mfanyabiashara wa Marekani Jamie Dinan na Alex Knaster ambaye ni mzaliwa wa Russia, linakaribia kukubali mpango wa kuinunua klabu hiyo ambayo thamani yake imewekwa kuwa dola 110 milioni za Kimarekani.
Kama watafanikiwa, Vialli atakuwa rais akiwa na mamlaka kamili ya uendeshaji katika menejimenti ya klabu hiyo.
Vialli aliichezea Sampdoria kuanzia mwaka 1984 hadi 1992 wakati enzi za dhahabu za klabu hiyo.
Nyota huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 55 aliiongoza Sampdoria kutwaa ubingwa wao pekee wa Serie A mwaka 1991, Kombe la Washindi na mataji matatu ya Kombe la Italia.
Alihamia Juventus mwaka 1992 na kuichezea klabu hiyo ya jijini Turin kwa misimu minne, akitwaa ubingwa wa Serie A na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kabla ya kuhamia Chelsea ya England.
Vialli pia alifunga mabao 16 katika mechi 59 alizoichezea Italia kabla ya kwenda kuzifundisha Chelsea na Watford.
Msimu uliopita, Sampdoria ilimaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tisa na inaanza kampeni ya msimu huu nyumbani kwa kuvaana na Lazio.

Advertisement