Ofisa Polisi Tanzania, wenzake wasomewa shtaka la kutakatisha fedha Sh798 milioni

Muktasari:

Ofisa wa Polisi, Emmanuel Mkilia(44), na wenzake watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha Sh798 milioni mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.

 

Dar es Salaam. Ofisa wa Polisi nchini Tanzania, Emmanuel Mkilia(44) na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kutakatisha fedha kiasi cha Sh798 milioni mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Mbali na Mkilia, washtakiwa wengine ni mtaalamu wa Tehama, Donald Mhaika (39) mkazi wa Kinondoni, Abdi Ally (48), mkazi wa Ilala na Mohyadin Hussein (56) mfanyabiashara na mkazi Mikocheni.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao, leo Januari 6, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Salum Ally.

Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka hao, hakimu Ally, alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Janeth Magoho, alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ta uhujumu uchumi namba 2/2020.

Simon alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 19, 2013 na Oktoba 18, 2013 Jijini Dar es Salaam, waliisababishia hasara Jeshi la Polisi Tanzania, kiasi cha Sh798 milioni.

Katika shtaka pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja na kwa njia ya udanganyifu walijipatia Sh798 milioni kutoka Jeshi la Polisi Tanzania.

Wakili Simon alidai kuwa washtakiwa hao walidai kuwa watafunga mfumo wa taarifa za watuhumiwa waliokamatwa na wanaoshikiliwa katika vituo vya polisi nane na kisha kutoa hati mbili ambazo zilionyesha kuwa wamefunga mfumo huo katika vituo vinne vya polisi, wakati wakijua sio kweli.

Katika shtaka la tatu, ambalo ni la kutakatisha fedha, wakili Magoho alidai siku na eneo hilo, washtakiwa walijipatia fedha kiasi cha Sh798.78 milioni wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka wamedai upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Hakimu Ally, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 20, 2020 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.