Ofisa mwingine polisi aunganishwa kesi kupokea rushwa ya Sh200 milioni

Muktasari:

  • Ofisa mpelelezi wa kituo cha Polisi Kawe, Emmanuel Njegele ameunganishwa na wenzake watatu katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh200 milioni.

Dar es Salaam. Ofisa mpelelezi wa kituo cha Polisi Kawe, Emmanuel Njegele ameunganishwa na wenzake watatu katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh200 milioni.

Mbali na Njegele, maofisa wengine wa watatu wa kituo hicho, Shaban Shillah, Joyce Kita na Ulimwengu Rashid walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 3, 2019.

Njegele ameunganishwa leo  na wenzake baada ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa hati ya kukamatwa ambapo amesomewa mashtaka tisa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Nickson Shao amemsomea mshtakiwa huyo makosa yanayomkabili ambayo aliyakana na kuelezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Mshtakiwa huyo alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Novemba 15, 2019 itakapotajwa tena.