Ofisi nyingine ya Serikali yachomwa moto Morogoro

Monday November 11 2019

 

By Lilian Lucas, Mwananchi

Morogoro. Watu wasiojulikana, wameichoma moto Ofisi ya Kijiji Cha Mlali kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro nchini Tanzania usiku wa kuamkia leo Jumatatu Novemba 11, 2019.

Aidha ofisi hiyo imechomwa moto pamoja na nyaraka zote zilizokuwa ndani ya ofisi hiyo zimeteketea kwa moto.

Uongozi wa mkoa wa Morogoro akiwemo Mkuu wa mkoa Loata Ole Sanare pamoja na kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa wako eneo la tukio wakifuatilia sababu za kuchomwa moto ofisi hiyo.

Mwananchi limemtafuta Sanare kuhusu taarifa hizo ambapo amesema yuko kwenye kikao eneo la tukio na kwamba atazungumza baadaye na waandishi wa habari.

Diwani wa Mlali, Frank Mwananziche amesema ofisi hiyo ilichomwa majira ya saa nane usiku na watu wasiojulikana.

Hii ni ofisi ya pili inachomwa moto baada ya watu wasiojulikana usiku wa kumakia jana Jumapili Novemba 10, 2019 kuichoma moto ofisi ya mtendaji wa kata ya Soweto katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Advertisement

Advertisement