VIDEO: PSSSF yawalipa mabilioni wastaafu 9,971 wa PSPF

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi na Ajira), Anthony Mavunde akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 11 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Fedha hizo ni malimbikizo ya deni la wastaafu 9,971 lililorithiwa na PSSSF kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF

Dodoma. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekamilisha kulipa Sh888.39 bilioni za malimbikizo ya deni la wastaafu 9,971 lililorithiwa kutoka Mfuko wa Pensheni wa PSPF.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 16, 2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga.

Katika swali lake la msingi, Haonga amesema watumishi wengi waliokuwa wanachama  wa PSPF wamestaafu zaidi ya mwaka mmoja lakini hawajalipwa fedha zao za kiinua mgongo na kusababisha waishi maisha ya tabu na kutaka kujua lini watalipwa fedha hizo.

“Mfuko umekamilisha mfumo wa ulipaji mafao utakaowezesha kufanya malipo katika ngazi ya mkoa hivyo kuwezesha kulipa mafao ya ndani ya muda uliowekwa kisheria wa siku 60 tangu mwanachama anapowasilisha madai,” amesema Mavunde.

Katika swali lake la nyongeza, Haonga amesema  kuwa mtumishi anapoajiriwa hujulikana wazi muda atakaostaafu na kuhoji sababu za Serikali kuchelewa kuwalipa pensheni zao.

“Sasa kwa kuchelewesha huku kwanini wasilipwe na riba maana wanaishi maisha ya tabu sana,” amehoji Haonga.

Katika majibu yake Mavunde amesema: “Kwa mujibu wa sheria mfuko unatakiwa kulipa mafao ndani ya siku 60, awali kulikuwa na changamoto ambazo nyingine zilitokana na wastaafu wenyewe taarifa zao kuwa na kasoro, ila  PSSSF wameweka utaratibu mzuri wa ulipaji.”