PanAfrican Energy yailipa serikali ya Tanzania malipo maalum ya kodi

Dar es Salaam. Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania Limited (PAET) leo Aprili 2, imeilipa serikali ya Jamhuri ya Muungano kodi ya nyongeza inayotokana na faida Sh 27.3 bilioni ($ 11.94 milioni).

Malipo hayo yameifanya PAET kuwa kampuni ya kwanza inayojishughulisha na mafuta pamoja na gesi kulipa aina hiyo ya kodi kwa serikali.

Akizungumza leo mkurugezI ttendaji wa PAET, Andy Hanna, amesema baada ya kuzalisha gesi asilia kwa zaidi ya miaka 15 wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutumia kipengele hicho maalum cha mkataba.

“ Linaweza kuonekana jambo geni kidogo kulizungumzia, lakini tunashukuru kwamba tumeweza kufanikiwa kutekeleza malipo haya makubwa na ya aina yake. Mpaka mwishoni mwa mwaka 2019, kampuni imeweza kuilipa serikali ya Tanzania kiasi cha Sh555 bilioni kama kodi mbali mbali na kiasi cha Sh 160 bilioni kama mgawanyo wa faida,” alisema Bw Andy.

Aliongeza:  Kodi ya Additional Profit Tax ambayo tumeilipa hivi karibuni inadhihirisha thamani ya kampuni yetu kwa wananch wa Tanzania, japo thamani sio tu kwa maana ya mapato.

Tofauti  na mikataba mingine ya uzalishaji wa gesi asilia, mkataba wa PSA wa Songo Songo umeweka kikomo kwenye kiwango cha faida ambacho kampuni husika Inaweza kukipata.

Chini ya PSA, kampuni ikisharudisha gharama zake za uendeshaji na kulipa kodi zote stahiki kwa mujibu wa sharia za nchi, faida inayobaki inagawanywa na serikali ya Tanzania kwa kuzingatia matakwa ya mkataba.

 Mkataba wa aina hii ni wa kawaida na umekuwa ukitumika katika mataifa mengine mengi duniani kote.

PAET, inazalisha gesi kutoka Songo Songo na kuisafirisha mpaka jijini Dar es Salaam ambapo hutumika katika shughuli za kuzalisha umeme.

Gesi hiyo pia inatumika kuendesha shughuli za uzalishaji katika viwanda vikubwa zaidi ya 40 jijini Dar es Salaam pamoja na kusambaza gesi asilia iliyogandamizwa  (Compressed Natural Gas ) kwa ajili ya kutumika kwenye hoteli,  viwanda na kwenye magari.

Mkataba wa uzalishaji  wa gesi asilia ya Songo Songo (PSA) yaani ulitiwa saini mwaka 2001 baina ya Serikali ya Tanzania na PAET.

 Mbali na mambo mengine, mkataba huo  unatoa muongozo wa namna uzalishaji wa gesi unavyopaswa kufanyika pamoja na jinsi mgawanyo wa mapato unavyopaswa kuwa baina ya pande hizi mbili.

Mkataba wa PSA unaweka matakwa kadhaa kwa PAET ambayo yote yamekuwa yakitimizwa tangu mkataba ulivyoanza.

Hata hivyo, kufanikisha hili na wakati huohuo kuendeleza shughuli za uzalishaji umehitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.

Taarifa iliyotolewa na PAET inasema Katika kipindi cha mkataba, kampuni imechimba visima vipya vya gesi na kufanikiwa kukarabati vile ambavyo vilichimbwa tangu mwaka 1974.

Pia kampuni imewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi asilia kupitia Shirika la Ugavi Umeme nchini Tanzania (Tanesco).