Pete tegesha chanzo cha Ukimwi kwa wanafunzi

Mwanza. Takwimu za maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nchini zimeshuka kutoka watu 100,000 kwa mwaka kwa miaka 10 iliyopita hadi watu 72,000 ingawa vijana wameendelea kuongoza kwa maambukizi.

Chanzo kikubwa cha vijana kupata maambukizi hasa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu kimetajwa kuwa ni ndoa tegesha na pete za uchumba.

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) Dk Leonard Maboko amesema kila mwaka zaidi ya vijana 28,000, sawa na asilimia 40 ya maambukizi mapya 72,000 huambukizwa VVU.

“Vijana wengi walioambukizwa wana umri wa miaka 15 hadi 24, wengi wao wakiwa wa kike,” alisema Dk Maboko katika kilele cha maadhimishi ya Siku ya Ukimwi duniani jijini Mwanza jana.

Awali, mkurugenzi wa shirika la Kivulini la jijini Mwanza linalotetea haki za wanawake na watoto, Yassin Ally alisema vijana wengi hasa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu huambukizwa VVU kutokana na tamaa ya kuolewa na kuishi maisha ya mitandaoni. “Wanafunzi wa kike vyuo vikuu hujikuta wakivishwa pete tegesha za uchumba. Wanapiga nazo picha na kuposti mitandaoni. Baadhi yao wanafunga hadi ndoa na kuishi kinyumba na wanaume ambao huwapa ujauzito na wakati mwingine kuwaambukiza Ukimwi kisha kuwatelekeza,” alisema.

Ndoa tegesha ni mbinu inayotumiwa na baadhi ya wanaume kuwadanganya wasichana kwamba wana nia ya kufunga nao ndoa na kuwavalisha pete kumbe nia yao ni kustarehe nao tu.

Kundi la wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili ndilo liko hatarini zaidi kurubuniwa kwa ndoa tegesha.

Serikali yashtuka

Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Jenista Mhagama imetangaza mpango wa kukabiliana na pete za uchumba na ndoa tegesha katika taasisi za elimu ya juu ili kuwanusuru wanafunzi wa kike ambao ndio waathirika wakuu.

“Taarifa hizi zimetushtua. Tumekubaliana na Waziri wa Afya kuitisha kikao cha wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi, ukatili na unyanyasaji kijinsia Januari 2020 ili kuweka mikakati ya kukomesha suala hili,” alisema.

Wanaume na michepuko

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Leticia Kapela alisema tabia ya baadhi ya wanaume kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengi ni moja ya sababu inayowafanya waogope kupima VVU.

“Baadhi ya wanaume wana michepuko inayoweza kujaa mabasi mawili. Hawa hawawezi kwenda kupima VVU wanajihofia wenyewe, badala yake wanajipima kupitia vipimo vya wake au wapenzi wao wakati wa ujauzito,” alisema Leticia.

Mashine za kujipima

Akizungumzia umuhimu wa kupima na kujua afya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema zaidi ya watu 17, 000 wamepima wenyewe na kujua afya zao kwa mashine maalumu baada ya kuwa miongoni mwa watu 26, 000 waliohusishwa kwenye utafiti na majaribio.

Wanaoishi na VVU

Kaimu meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk James Kamuga alisema kufikia Septemba 2019 zaidi ya watu 1.2 milioni kati ya watu 1.6 milioni waliokadiriwa kuishi na VVU wameingizwa kwenye huduma ya dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi zinazotolewa bure na Serikali

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na VVU (Nacopha), Leticia Kapela aliishukuru Serikali kwa kutoa bure dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi akisema bila kufanya hivyo wengi wa wanaoishi na VVU wangepoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za kununua dawa.

Imeandikwa na Peter Saramba, Jesse Mikofu na Sada Amir