Picha ya Erick Kabendera yatumika maziko ya mama yake, Padre atoa ujumbe

Muktasari:

Mwili wa Verdiana Mujwahuzi (80), mama mzazi wa mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera aliyefariki dunia Desemba 31, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Amana jijini Dar es Salaam umezikwa jana Jumatatu Januari 6, 2019 Kijiji cha Kashange kata ya Katoma Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Tanzania.

Bukoba. Safari ya mwisho hapa dunia ya Verdiana Mujwahuzi ambaye ni mama mzazi wa mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick Kabendera ilihitimishwa jana Jumatatu Januari 6, 2020.

Mwili wa Verdiana aliyefariki dunia Desemba 31, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Amana jijini Dar es Salaam ulizikwa kijiji cha Kashange kata ya Katoma Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera na kuhudhuriwa na mamia ya watu.

Pande wa Kanisa Katoliki Fortunatus Rutaihwa aliongoza ibada aliongoza ibada ya maziko ya marehemu huku akiionya jamii kuepuka kusababisha kifo cha mtu yeyote kwa sababu ya kuonea na dhuluma.

Katika mahubiri yake wakati wa, Padre Rutaihwa ambaye ni paroko kutoka Seminari ya Rubya mkoani Kagera aliisihi familia na wote wenye mapenzi mema kumwombea Erick anayesota mahabusu aya Segerea Dar es Salaam akisema Mungu husikiliza na kujibu kilio cha mnyonge.

Kabendera yuko mahabusu tangu Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ikiwamo la uhujumu uchumi na utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh173 milioni.

Huku akisikilizwa kwa makini na umati uliohudhuria mazishi hayo, Padre Rutaihwa alisema ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kuwaombea rehema wote wanaoonewa, kunyanyaswa na kudhulumiwa ili Mungu atende sawasawa na mapenzi yake.

"Naisihi familia na watu wote kumlilia na kumwombea Erick katika yote yanayomkabili kwa sababu Mungu husikia kilio cha wanyonge na wanaoonewa," alisema Padre Rutaihwa

Akitoa salaam kwa niaba familia,  Rose Baregu aliwashukuru wote walioshirikiana na familia kwa njia moja au nyingine kuanzia jijini Dar es Salaam hadi Bukoba na kufanikisha shughuli zote za msiba na mazishi ya mama Verdiana.

Akisoma ujumbe wa Erick unaofanana na ule uliosomwa wakati wa misa jijini Dar es Salaam,  Wakili wa mwandishi huyo,  Jebra Kambole alisema licha ya kuwa mahabusu, Erick aliahidi kuwa pamoja kiimani na ndugu, jamaa na marafiki wakati wa mazishi hayo.

Muda wote wa misa,  picha kubwa ya Erick iliwekwa kwenye kiti alichostahili kuketi katikati ya watoto wa marehemu Verdiana. Baadaye picha hiyo ilibebwa na mmoja wa wanafamilia aliyekalia kiti hicho.

Picha hiyo ni iliyopigwa Januari 2, 2020 Mahakama ya Kisutu siku kesi yake ilipotajwa pamoja na kuwasilisha maombi ya kuruhusiwa kwenda kuaga mwili wa mama yake kesho yake yaani Januari 3, 2020 katika Kanisa Katoliki Chang’ombe, Dar es Salaam.

Katika picha hiyo, inamwonyesha Kabendera akiwa ameinama, akitumia kitambaa chake kujifuta usoni.

Hata hivyo, uamuzi uliotolea na Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Janeth Mtenga ilimzuia Kabendera kwa hoja kwamba haina mamlaka ya kusikiliza ombi hilo hadi kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Akizungumza kwa niaba ya marafiki wa Kabendera wa ndani na nje ya Tanzania, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisisitiza kauli ya Padre Rutaihwa akiwaomba Watanzania kila mmoja kwa imani yake kumwombea Kabendera huku akisifia umoja, mshikamano na undugu ulioonyeshwa na watu wakati wa msiba huo.

"Watanzania tumedhihirisha hulka na utamaduni wetu wa kushirikiana bila kujali tofauti zetu kisiasa, kidini na kijamii. Mimi natoka mkoa wa Kigoma lakini niko hapa kumsindikiza mama Verdiana ambaye ni mama Erick ambaye kwangu siyo rafiki bali ndugu," alisema Zitto

Wengine waliohudhuria maziko hayo ni ni waziri wa zamani wa maliasili na utalii wa Tanzania, Balozi Khamis Kagasheki, Meya wa Manispaa ya Bukoba, Chief Karumuna, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Dk Rugemeleza Nshala, waandishi wa habari, ndugu, jamaa na marafiki.