Polepole azungumzia maridhiano yanayoombwa na wapinzani

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema vyama vya upinzani nchini Tanzania  vimeshindwa kuzingatia hatua za msingi na awali kabla ya kufikia hatua ya maridhiano.

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema vyama vya upinzani nchini Tanzania  vimeshindwa kuzingatia hatua za msingi na awali kabla ya kufikia hatua ya maridhiano.

Polepole alitoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka 43 ya CCM wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro yaliyobeba kauli mbiu ya ‘Tuliahidi, Tumetekeleza na tunaahidi tena kuchapa kazi kwa juhudi, ubunifu na maarifa zaidi’.

Polepole ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho vyama vya upinzani hasa Chadema, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi vikitaka meza ya mazungumzo ili mambo mbalimbali yanayolalamikiwa yatatuliwe.

Katika sherehe hizo, Polepole amesema amekuwa akifuatilia a mijadala na mapendekezo yaliyotolewa na vyama vya upinzani kuhusu maridhiano.

“Maridhiano ni hatua na vyama vya upinzani nchini vimeshindwa tangu mwanzo kuzingatia hatua za msingi na za awali,  na hata sasa kabla ya kufikia hatua ya maridhiano.”

“Hilo linawakosesha uhalali wa kutaka maridhiano, kwa sababu maridhiano huanza kwa kuwa na uelewa wa pamoja katika mambo ya msingi, pili kujenga muafaka na tatu kuwa na maridhiano yenyewe,” alisema Polepole

 Akifafanua kuhusu dhana na nadharia ya maridhiano, Polepole amesema kuwepo kwa uelewa wa pamoja kujua Watanzania wanataka nini, kazi kubwa ya maendeleo ambayo imekwisha kufanyika nchini na kubadilisha kabisa hali na ustawi wa watu.

“Muafaka wa kitaifa kwa maana ya kukubaliana katika kazi nzuri ambayo imefanyika na katika yale ambayo hakuna muafaka ndio tunakwenda katika maridhiano,” amesema.

Polepole alitumia nafasi hiyo pia kuelezea ni namna gani CCM i kimejipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 huku akiangazia mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 43.