VIDEO: Polisi Morogoro wakamata dawa za kulevya, raia wa kigeni

Muktasari:

  • Raia watano wa Ethiopia wamekamatwa na polisi mkoani Morogoro wakisafirishwa kwenda Afrika Kusini.

Morogoro. Raia watano wa Ethiopia wamekamatwa na polisi mkoani Morogoro wakisafirishwa kwenda Afrika Kusini.

Polisi pia wamekamata bangi magunia tisa, madumu mawili ya lita 20 yakiwa yamejaa bangi, gari moja aina ya Prado na pikipiki moja zilizokuwa zikisafirisha bangi hizo na dawa za kulevya aina ya Heroin gramu 29.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 21, 2020 kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Mugabo Wekwe amesema Februari 19, 2020 walipata taarifa za watu kusafirisha bangi.

Amesema waliweka mtego katika barabara kuu ya Morogoro- Dar es salaam na kukamata gari lililokuwa likiendeshwa na Jaffunery Jaji  maarufu Emanuael akiwa na Modest  Salim.

Amebainisha walipofanya upekuzi walikuta bangi zikiwa katika magunia nane ya kilo 150.17, “gari ilikuwa na namba bandia ili wapate urahisi wa  kusafirisha bangi. Walikuwa wakitokea Doma wilayani Mvomero kwenda Dar es salaam.”

Amesema katika tukio jingine la Februari 19, 2020 eneo la Nanenane polisi walimkamata Chesco Emanuel akiwa na madumu mawili ya maji ya lita 20 yaliyokuwa yamehifadhi bangi yenye uzito wa kilo 7.4. amesema ilikuwa ikisafirishwa kutoka Mlali, Morogoro kwenda  Mkambarani.

Amesema Februari 12, 2020 maeneo ya Matombo, Morogoro polisi walimkamata Maganga Kaji akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin zilizohifadhiwa kwenye mifuko laini.

Amebainisha kuwa Februari 20, 2020  maeneo ya Green barabara kuu ya Morogoro- Iringa waliwakamata Jafari Mshana akiendesha gari aina ya Toyota Cresta akiwasafirisha wahamiaji watano raia wa Ethiopia.

Amewataja raia hao wa Ethiopia kuwa ni Mulken Tesfaye, , Samuel Wamebo, Mohamed Amani, Abdilsalme Amsny na  Solomon Demekwe wakiwa hawana hati za kusafiria na wawili kati yao walifungiwa kwenye  nyuma ya gari na watatu wakilazwa nyuma ya kiti cha dereva.

Amesema Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mahojiano yatakapokamilika.