Polisi Mwanza yawashikilia 46 tuhuma mbalimbali ikiwamo mauaji

Muktasari:

Kwa kipindi cha miezi miwili kati ya Julai na Septemba, 2019 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata zaidi ya watu 46 kwa tuhuma za kufanya vitendo vya uhalifu ndani na nje ya jiji kutokana na operesheni mbalimbali zinazoendelea.

Mwanza. Polisi Mkoa wa Mwanza nchini Tanzania limewakamata watu 46 kwa makosa manne tofauti likiwemo la mauaji na wizi wa transfoma ya umeme mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Ndani ya kipindi cha miezi miwili zaidi ya watu 96 wamekamatwa na polisi mkoani humo kwa tuhuma za vitendo vya uhalifu mbalimbali kutokana na operesheni zinazoendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Septemba 22, 2019 Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Jumanne Muliro amesema tukio la kwanza wanashikiliwa watu wanne kwa tuhuma za kumuua askari mgambo Nickson Mabuku.

Amesema tukio hilo lilitokea jana Jumamosi katika Kisiwa cha Bezi wilayani Ilemela ambapo walimshambulia mgambo huyo wakati akitekeleza majukumu yake wakipinga kitendo cha kukamatwa Laurent Joseph kwa tuhuma za wizi.

“Walimshambulia kwa silaha za jadi kisha kumzamisha ziwani na kusababisha kifo chake,” amesema kamanda Muliro

Katika tukio la pili, Kamanda Muliro amesema wamewakamata watu wawili wakiwa na transfoma mali ya Tanesco eneo la Mwaloni Kirumba ambayo iliibwa katika wilaya ya Sengerema.

Pia, kamanda Muliro amesema wamewakamata watu 28 wakiwa na betri za minara ya simu, televisheni mbalimbali, kompyuta mpakato, injini za boti, deki na nyavu 15 za kuvulia samaki.

Kamanda huyo amesema katika msako ulioza Septemba 16 hadi 21, 2019 wamekamata watuhumiwa 12 wanaojihusisha na utengenezaji, uuzaji, unywaji wa pombe haramu ya moshi ambapo walikamata lita 110, mitambo mitano na mapipa sita ya pombe hiyo.

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa 23 kati ya 46 wameshafikisha a mahakamani na kesi zao zinaendelea.