Polisi Tanzania wakamata magari ya wizi 130, pikipiki 193

Muktasari:

Jeshi la Polisi Tanzania linaendelea na mahojiano ya watuhumiwa 128 ya matukio mbalimbali ya magari, pikipiki na vipuli vyake vilivyoibiwa katika kipindi cha Januari na Februari 2020.

Dodoma. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limekamata magari 130, pikipiki 193, vipuri mbalimbali vya magari na pikipiki 753 katika operesheni iliyoendeshwa nchi nzima.

Akizungumza leo Jumamosi Machi 28, 2020 Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI) Robert Boaz amesema wanawahoji watuhumiwa 128 na pindi upelelezi utakapokamilika sheria itachukua mkondo wake.

“Wanunuzi wa magari yaliyotumika ni muhimu kabla ya kununua wajiridhishe muuzaji ni mmiliki halali kwa kutumia polisi kukagua gari hilo na taarifa hizo kuoanisha na kadi pamoja na kumbukumbu zilizopo kwenye mfumo wa TRA (Mamlaka ya Mapato Nchini),” amesema Boaz

Pia, amewataka wamiliki wa magari wanaotaka kufanya mabadiliko makubwa kwenye magari yao ikiwamo kubadilisha injini, rangi ni lazima watoe taarifa TRA ili mabadiliko hayo yafanyike kwenye kumbukumbu za gari zilizopo kwenye mfumo wa TRA.

Boazi amewataka wauzaji wa vipuri vikuu kuu kuzingatia sheria na kanuni zinazowataka kuwa na leseni halali na kuweka kumbukumbu za kuonyesha walipopata vipuri hivyo ili kujiepusha na usumbufu, uchanjaji wa magari pamoja na kupokea mali za wizi.