VIDEO: Polisi Tanzania wamkamata Profesa Lipumba

Muktasari:

Polisi Mkoa wa Tanga nchini Tanzania wamemkamata Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini humo cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwa madai ya kufanya ziara wilayani Handeni bila kupewa kibali. Profesa Lipumba amepelekwa Kituo cha Polisi Handeni.

Handeni. Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amekamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Handeni Mkoa wa Tanga akidaiwa kufanya ziara bila kupewa kibali.

Profesa Lipumba amekamatwa leo Jumapili Januari 26, 2020 Kijiji cha Segera wilayani Handeni na kupelekwa kituo kikuu cha polisi wilayani humo kilichopo mjini Handeni.

Mkurugenzi wa Usalama wa CUF, Masoud Mhina amesema mwenyekiti huyo amekamatwa wakati akijiandaa kufungua tawi la chama hicho Kijiji cha Segera.

Amesema ameshangazwa na kitendo hicho cha polisi kumkamata Profesa Lipumba wakati tayari chama kilishawasilisha jeshi la polisi taarifa ya ziara hiyo.

Amesema Profesa Lipumba leo Jumapili ilikuwa anamaliza ziara yake ya siku saba mkoani Tanga na baada kumaliza mkutano wa ndani wa kijiji cha Mkata na kisha kwenda jijini Dar es Salaam.

Profesa Ibrahim Lipumba alianza ziara yake mkoani Tanga Jumapili iliyopita ambapo alianza Pangani, Mkinga, Muheza, Korogwe, Lushoto na leo alikuwa amalizie Handeni.

Jitihada za  kumpata Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe zinaendelea ili kujua undani wa Polisi kumkamata Mwenyekiti huyo wa CUF.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi