Polisi Tanzania yamhoji baba wa mwanafunzi aliyejiua kwa risasi

Muktasari:

Polisi mkoa wa Arusha nchini Tanzania wamemuhoji baba wa mwanafunzi anayedaiwa kujiua kwa kujipiga risasi  jijini Arusha. Baada ya mahojiano hayo polisi wamemwachia.

Arusha. Polisi mkoani Arusha nchini Tanzania limemkamata na kumuhoji Salim Ibrahim (56) ambaye ni baba wa mwanafunzi, Faisal Salimu (19) aliyejiua kwa kujipiga risasi jana Jumapili alfajiri Agosti 18,2019.

Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Jonathan Shana akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 19,2019 amesema baada ya mahojiano polisi imemwachia Ibrahim.

"Tulimchukua kwa mahojiano baba wa mtoto huyu na baada ya uchunguzi wa awali tumemwachia na uchunguzi unaendelea," amesema Shana.

Hata hivyo, amesema sheria zipo kwa watu wanaomiliki silaha kutakiwa kuhifadhi vyema silaha zao.

Mwanafunzi huyo wa kidato cha tano, Shule ya Arusha Meru alijiua kwa kujipiga risasi kwenye paji la uso akiwa chumbani kwake katika nyumba anayoishi na baba yake pekee mkoani Arusha.

Tayari mwili wa mwanafunzi huyo umezikwa jana Jumapili.

Mwanafunzi huyo mwenye asili ya Kiasia alijiua kwa risasi kwa kutumia bunduki aina ya Rifle Winchester  akiwa amejifungia chumbani kwake katika nyumba ya Shirika la Nyumba za Taifa (NHC) plot namna 3 na 4 nyumbani kwao eneo la soko kuu jijini Arusha.