Polisi bado wanachunguza sakata la Idris Sultan

Muktasari:

Benedict Ishabakaki ambaye ni  mwanasheria wa msanii wa vichekesho nchini Tanzania,  Idris Sultan amesema bado polisi wanachunguza kosa linalomkabili mteja wake.

Dar es Salaam. Benedict Ishabakaki ambaye ni  mwanasheria wa msanii wa vichekesho nchini Tanzania,  Idris Sultan amesema bado polisi wanachunguza kosa linalomkabili mteja wake.

Alhamisi iliyopita Oktoba 31, 2019 Idris alihojiwa kwa saa tano na polisi na kupekuliwa nyumbani kwake kisha kuachiwa kwa dhamana akidaiwa kujifananisha na mtu mwingine na kuchapisha taarifa za uongo.

Aliripoti polisi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Alipoachiwa kwa dhamana aliripoti polisi Ijumaa Novemba Mosi, 2019 kutakiwa kuripoti tena leo Jumatano Novemba 6, 2019.

Akizungumza na Mwananchi, Ishabakaki amesema  mteja wake alifika tena kituoni cha polisi kati leo saa 2 asubuhi na kujibiwa na polisi kuwa upelelezi bado haujakamilika.

 “Tulifika tena asubuhi kuripoti kwa ajili ya mteja wetu lakini tumeambiwa upelelezi bado haujakamilika hivyo tunasubiria Jumatatu ijayo polisi watatueleza walipofikia. Hadi sasa wameshikilia simu na kompyuta mpakato za mteja wangu,” amesema mwanasheria huyo.

Ilivyokuwa

Mkasa ulianza kama masihara kwa Idris kuweka katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia katika mtandao huo na kumtaka mchekeshaji huyo wa vituko vya ‘Sio Habari’ kujisalimisha polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Alipozungumza na Mwananchi baadaye kuhusu sakata hilo, Makonda alisema “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris iwapo atakamatwa, Makonda alisema “brother ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”