Polisi waanza uchunguzi kifo cha mwandishi wa habari

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala, Zuberi Chembela amesema wameanza  uchunguzi wa awali wa kifo cha mwandishi wa habari, Deogratius David aliyekutwa amekufa chumbani kwake eneo la Buguruni,  Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala, Zuberi Chembela amesema wameanza  uchunguzi wa awali wa kifo cha mwandishi wa habari, Deogratius David aliyekutwa amekufa chumbani kwake eneo la Buguruni, Dar es Salaam.

David alikuwa akifanya kazi ya kujitolea katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alikuwa amekufa jana Jumatatu Januari 27, 2020.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 28, 2020, Chembela amesema bado uchunguzi unaendelea na polisi hawawezi kutoa taarifa za chanzo cha kifo kwa sasa.

“Bado tunachunguza. Mwili umekutwa ndani kitu cha kwanza kufanya ilikuwa ni kuutambua mwili, mara ya mwisho aliingia nyumbani kwake lini. Bado tunachunguza hatuna maelezo yoyote kwamba mpaka sasa tumegundua nini.”

“Hizo ni taratibu za upelelezi  bado tunaendelea nazo, tunachokifanya sasa ni kuzungumza na majirani  watuambie marehemu walimwona mara ya mwisho lini na taarifa nyingine kuzunguka eneo,” amesema kamanda huyo wa polisi.

Mwili wa David ulipatikana baada ya mlango wa chumba chake kuvunjwa jana asubuhi kutokana na kuwepo kwa harufu kali kutoka katika chumba hicho.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa sharti la kutotajwa jina mmoja wa majirani amesema, “Deo hajaonekana  kwa siku kadhaa na kwenye simu hapatikani lakini kilichotupa wasiwasi ni harufu kali iliyokuwa inatoka kwenye chumba chake.”

“Asubuhi ya leo tukavunja mlango ndio alipokutwa akiwa kitandani kwake mwili ukiwa umeharibika vibaya, hilo ndilo linaloweza kusema kwa kifupi mengine watakuwa nayo polisi.”

Habari zaidi zinaeleza majirani walitoa taarifa polisi waliofika  eneo hilo na kuchukua mwili wa mwandishi huyo.

Mwili wa David unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda Sumbawanga kwa mazishi.