Polisi wachunguza madai kukamatwa kura feki Mwanza

Muktasari:

Kapu lenye kura zilizopigwa tayari, nyingi zikiwa za urais zimekamatwa zikiingizwa kwenye kituo cha kupiga kura cha Mbugani jijini Mwanza.

Mwanza. Kapu lenye kura zilizopigwa tayari, nyingi zikiwa za urais zimekamatwa zikiingizwa kwenye kituo cha kupiga kura cha Mbugani jijini Mwanza.

Kapu hilo lililodaiwa kubeba chakula cha mawakala wa chama kimoja likiwa na kura zlizopigwa tayari kwa mgombea urais kupitia chama hicho.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema polisi inachunguza ukweli wa tukio hilo, baada ya kuona kipande cha video kikizunguka kwenye mitandao ya kijamii.

“Nimeona clip (kipande cha picha) fulani inatembea; Sayansi siku hizi ni kubwa. Watu wanatengeneza vitu vya hapa na pale na unajua kipindi hiki ni cha hekaheka na njama mbalimbali. Kwa kifupi nafuatilia kujua kuna nini na ukweli wake,” amesema Kamanda Muliro

Tukio lilivyokuwa

Kura hizo ambazo idadi yake haikujulikana mara moja kutokana na askari polisi waliokuwepo eneo la tukio kulidhibiti kapu hilo pamoja na mwanamke aliyedaiwa kulileta kituoni hapo zilibainika baada ya viongozi wa Chadema kata ya Mbugani kupewa taarifa za kuwepo njama za kuingiza kura bandia kituoni hapo.

Akizungumza wakati wa kukamata kura hizo, Katibu wa Chadema kata ya Mbugani, David Tumaini amesema baada ya kupata taarifa hizo, yeye na viongozi wenzake waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mwanamke aliyekuwa na kapu hilo.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) kata ya Mbugani, Maseza Mohamed amesema kitendo cha mwanamke aliyekuwa na kapu hilo kuanza kubabaika kiliwalazimisha kumweka chini ya ulinzi na kuita askari polisi.

“Polisi walipofika na kumhoji alidai ndani ya kapu kuna chakula na maji kwa ajili ya mawakala wake, lakini tulipoangalia tutakuta kura za Urais ambazo tayari zimepigwa kwa mgombea wa CCM,” amesema Maseza

Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Jofrey Kavenga amesema chama hicho hakijapata taarifa za kada wake kukamatwa akidaiwa kujaribu kuingiza kura zilizopigwa tayari kituoni na kuahidi kufuatilia suala hilo kubaini ukweli.

"Bado sijapata taarifa hizo; labda kwa sababu umeniuliza ngoja sasa nizifuatilie kujua ukweli," amesema Kavenga.