Polisi wachunguza video inayodaiwa kuwa ya Gwajima

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kwa kushirikiana na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), wameanza uchunguzi wa video ya ngono inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidhaniwa kuwa ni ya mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), limeanza uchunguzi wa video ya ngono inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidhaniwa kuwa ni ya mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Taarifa ya polisi imetolewa leo kufuatia kusambaa kwa video hiyo inayodaiwa kuwa ni yake, ikimuonyesha akiwa faragha na mwanamke.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatano, Mei 8, 2019 na Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, imeeleza kuwa Mei 7,2019 kuna video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wasiojulikana ikionyesha mtu anayefanana na mchungaji huyo akiwa na mwanamke asiyefahamika.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limeanza uchunguzi wa video hiyo mara moja na linapenda kuwapa taarifa wananchi (kuwa) Gwajima siyo mtuhumiwa, ni muathirika wa tukio hilo kwani tukio hilo linaweza kufanywa na mtu yeyote kwa nia ya kutaka kuharibu heshima yake kwa jamii na waumini," amesema Mambosasa.

Taarifa hiyo imesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza video hiyo kwa maelezo kuwa ni kosa la jinai na kuwataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu kwani uchunguzi unaendelea ili kubaini aliyeisambaza na lengo la kufanya hivyo.