Polisi wanaodaiwa kubambika kesi ya utakatishaji washitakiwa kijeshi

Moshi. Askari Polisi wa kituo cha Himo wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wanaotuhumiwa kufanya jaribio la kumbambikia raia mmoja, kesi ya kutakatisha fedha, wamefunguliwa mashitaka ya kijeshi.

Polisi hao na watu wengine watatu, ambao miongoni mwao wawili hawajakamatwa, wanadaiwa kujifanya maofisa usalama wa Taifa waliotumwa kumkamata raia huyo, na baadaye kumdai Sh140 milioni ili wamwachie huru.

Baada ya taarifa hizo kuandikwa na Mwananchi, polisi hao walikamatwa Januari 6 pamoja na mfanyakazi wa zamani wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa) na kushikiliwa na polisi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Salum Hamdun alipoulizwa jana alisema kuanzia Januari 6, polisi hao walikuwa wakishikiliwa mahabusu wakati jeshi hilo likifanya uchunguzi wake.

“Tulikuwa tunafanya uchunguzi wa hizi tuhuma. Uchunguzi umekamilika sasa hivi tuko katika hatua za kiutawala kwa maana ya mashitaka ya kijeshi dhidi ya hawa askari.

“Mwenendo wa mashitaka na `facts’ (ukweli) ndizo zitakazo ‘determine’ (kuamua) adhabu watakayopewa. Walikuwa mahabusu wakati uchunguzi unaendelea leo (jana) tumewaachia kwa dhamana.” Askari hao wameachiwa baada ya kusota mahabusu siku 18

Januari 2 huko karibu na lango kuu la kuingia Kinapa, mmoja wa watuhumiwa ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa mamlaka hiyo, alimfuata raia huyo akimshawishi ambadilishie fedha za kigeni.

Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara huyo, Julius Mlay alidai siku ya tukio alifika mtu aliyewahi kuwa askari wa Kinapa kabla ya kufukuzwa kazi, akaomba ambadilishie Dola 100 za Marekani.

“Huyo bwana namfahamu kwa hiyo akaniambia ana wageni wake wanataka kwenda ‘day trip’ (matembezi ya siku moja) na hana hela ya Tanzania ambayo anatakiwa kuweka kwenye simu,” alidai.

“Utaratibu ni kuwa huwezi kulipa `cash’ (fedha taslimu) getini kwa hiyo akaomba nimpe Sh220,000 aniachie ile dola 100 na baada ya wageni wake kupanda na kushuka angechukua dola zake”.

Mfanyabiashara huyo anadai ghafla wakati amempa fedha hizo kwa ahadi atazirudisha na kuchukua dola yake, walitokea watu hao watano waliojitambulisha ni maofisa usalama wa Taifa.

“Walinikamata na kuniambia watu kama mimi ndio Rais Magufuli anawatafuta washitakiwe kwa utakatishaji fedha. Wakasema nitakaa gerezani miaka mitano ndio nihukumiwe,” alidai.

Lakini alidai kabla ya kuondoka eneo hilo, walifanya upekuzi katika ofisi yake na kukuta Sh2 milioni kwenye droo ambazo walizichukua na kumweleza anatakiwa kusafirishwa kwenda Dar.