Polisi wasema aliyehusika Mangula kupewa sumu atasakwa ndani, nje ya CCM

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linafanya uchunguzi kubaini sababu makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula kuwa na sumu mwilini.

Dar es salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linafanya uchunguzi kubaini sababu makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula kuwa na sumu mwilini.

“Tunachunguza kubaini sumu iliingiaje mwilini mwake,” amesema Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 9, 2020.

"Uchunguzi kuhusu namna sumu hiyo ilivyoingia mwilini bado unaendelea kufanyika. Polisi watachukua hatua kali

kwa mtu yoyote atakayebainika kupanga, kuratibu au kutekeleza uhalifu huo. Awe ni mwanafamilia kutoka ndani ya chama, nje ya chama, ndani ya nchi au nje ya nchi. Awe serikalini au chama chochote cha siasa.”

Februari 28, 2020 Mangula alianguka katika kikao cha kamati kuu ya CCM kilichofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.

Mambosasa amesema Machi 2, 2020  walipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa CCM kuhusu Mangula kuwekewa sumu.

“Polisi kwa  kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na taasisi mbalimbali baada ya kufanya uchunguzi walibaini kwenye mwili wa Mangula kulikuwa na sumu,” amesema Mambosasa.

Jumamosi ya  Februari 29, 2020  Rais wa Tanzania, John Magufuli alimjulia hali Mangula aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuanguka ghafla Ijumaa Februari 28, 2020.

Taarifa ya Mangula kuugua ilitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa huku video zikimuonyesha Magufuli akizungumza naye, baadaye kusali pamoja.

Mangula alionekana akiwa amelala kitandani huku akiwa na plasta juu ya jicho lake la kushoto.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Mangula ambaye  alishiriki kikao cha kamati kuu ya chama hicho sambamba na Magufuli  kilichofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba Februari 28, 2020, baada ya kuanguka alilazwa chumba cha uangalizi maalum (ICU).

“Mangula aliugua ghafla jana na kisha kukimbizwa hospitali kwa matibabu,” inaeleza taarifa hiyo.

“Utapona na Mungu atakusimamia katika tatizo hili, sisi tulipoona jana (Ijumaa Februari 28, 2020)  umeanguka ilitushtua,” amesema Magufuli na Mangula kujibu, “sijui nimeangukaje.”

 “Huwezi  ukajua ila sisi tunamkabidhi Mungu na Mungu atakusimamia, Mungu akujalie sana,” amesema Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

Katika kikao hicho cha kamati kuu, yalijadiliwa masuala mbalimbali zikiwemo adhabu za makatibu wakuu wa zamani, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Katika maazimio hayo, Makamba alisamehewa, Kinana aliwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 18 na kutakiwa kutogombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho huku Membe akifukuzwa uanachama.