Polisi wazuia kongamano la CUF mkoani Tabora

Wednesday October 9 2019

 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Tabora. Jeshi la polisi Mkoa wa Tabora limezuia kongamano la Chama cha Wananchi (CUF) lililokuwa lifanyike leo Jumatano Oktoba 9, 2019 Wilaya ya Tabora.

Mbali na kuzuia kongamano hilo, pia wamezuia ufunguzi wa matawi ya chama hicho wilayani humo uliokuwa ufanyike kesho Alhamisi.

Kongamano hilo ni mwendelezo wa ziara ya mwenyekiti wa CUF,  Profesa Ibrahim Lipumba kuimarisha chama hicho na kuhamasisha uandikishaji wa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Jana Jumanne Oktoba 8, 2019 kamanda wa polisi Wilaya ya Tabora alikiandikia barua chama hicho akikitaka kutofanya shughuli hizo.

Barua hiyo inaeleza kuwa kutokana na tathmini ya hali ya ulinzi na usalama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa katika jamii kuna mihemko ya kisiasa inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

"Kwa mazingira hayo na kwa nia njema yakuendeleza amani na utulivu bado mikutano ya nje ya kisiasa hairuhusiwi kwa kipindi hiki na hatuna pingamizi na mikutano ya ndani,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Advertisement

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora,  Barnabas Mwakalukwa amesema polisi haijazuia  mikutano ya ndani ila kilichozuiwa ni ufunguzi wa matawi.

"Mkishakusanyika zaidi ya  mmoja tayari ni mkutano wa hadhara ufunguzi wa matawi unakuwa na shamrashamra ila wakikaa kikao cha  ndani sina shida,” amesema Mwakalukwa

Mkurugenzi wa habari na mahusiano ya umma wa CUF,  Abdul Kambaya amesema kinachofanyika si mkutano wa hadhara bali ni ufunguzi wa matawi, kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi, si sehemu ya wazi.

Advertisement