Precision Air yatoa tiketi 120 kwa CCBRT kufanikisha huduma kwa wote

Wednesday September 11 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Precision Air limetoa tiketi za ndege kwenda na kurudi safari 120 kwa hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ili kusaidia kufikisha huduma za hospitali hiyo kwa watu wenye uhitaji katika mikoa mbalimbali nchini humo.

Leo Jumatano, Septemba 11, 2019 shirika hilo limesaini mkataba wa makubaliano na CBRT kuwapatika tiketi hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh60 milioni ambazo zitakuwa zikitumika kwa safari za kutoa au kuboresha huduma kwa watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Precison Air, Patrick Mwanri amesema mkataba huo wa mwaka mmoja ni sehemu utaratibu wa kampuni kurudisha kwa jamii na baada ya hapo kama kutakuwa na matokeo chanya unaweza kuwa endelevu lengo ni kuhakikisha ustawi wa Watanzania.

"Kama shirika tuna jukumu la kutunza na kufanikisha mahitaji ya jamii inayotuzunguka na tunaweza kufanya hivyo kupitia huduma tunazozitoa, tiketi hizi zinaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya," amesema Mwanri.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda Msangi amesema tiketi hizo zitasaidia kusogeza huduma zaidi kwa makundi yanayohudumiwa zaidi na hospitali hiyo ambao ni wagonjwa wa macho, vipimo, mifupa, fistula na ugawaji wa baiskeli kwa gharama nafuu.

"CCBRT husafiri kwenda katika mikoa mbalimbali kutoa huduma, wafanyakazi wetu husafiri kwa ajili ya kufanikisha hilo lakini pia huwa tuna vipindi vya kuwajengea uwezo madaktari wa vituo vya Serikali ili wenye uhitaji wasilazimike kuja Dar es Salaam, ushirika huu na  Precision Air utatuongezea ufanisi zaidi," amesema Msangi.

Advertisement

Anasema CCBRT ina vituo katika mikoa ya Iringa, Kigoma, Kilimanjaro na Tabora lakini baada ya kupata ufadhili huo watapata fursa ya kutoa huduma katika mikoa mingine.

Advertisement