Profesa Kabudi, Saashisha wanusurika ajalini

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, saa nane mchana katika Barabara Kuu ya Moshi kwenda Arusha maeneo ya uzunguni wilayani humo.

Morogoro/Moshi. Wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa) na Saashisha Mafuwe (Hai) wamenusurika kifo baada ya kupata ajali ya gari katika maeneo tofauti hivyo kufanya idadi ya wagombea waliopata ajali ndani ya wiki tatu kufika sita.

Wagombea wengine waliopata ajali katika kipindi hicho ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Ado Shaibu (Tunduru Kaskazini), Fuata Nabaraka (Mtwara Vijijini) na Said Bakema (Kigoma Kusini). Wagombea wote wanne wanawania ubunge kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

Profesa Kabudi ambaye ni waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki alipata ajali hiyo saa tatu asubuhi na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Morogoro kwa uchunguzi, hata hivyo inaelezwa kuwa anaendelea vizuri.

Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa hospitalini hapo, mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bajaji aliyekatiza ghafla barabarani na kusababisha gari la Profesa Kabudi kugongana na jingine.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu ajali hiyo na baada ya kuukamilisha taarifa rasmi ya chanzo cha ajili hiyo itatolewa na kamanda wa mkoa.

Ole Sanare alisema Profesa Kabudi yupo salama, hana majeraha yoyote isipokuwa maumivu kidogo hata hivyo madaktari wamempumzisha ili kufuatilia afya yake kwa ukaribu zaidi.

“Mimi mwenyewe nimemwona na nimeongea naye, yupo safi kabisa. Naomba wananchi hususan wa Kilosa waniamini, ninawahakikishia muda si mrefu atainuka na kuendelea na shughuli zake,” alisema Ole Sanare.

Ole Sanare alisema alipata taarifa za ajali hiyo akiwa ziarani Kilosa na kufafanua kwamba Kabudi alikuwa akitoka jimboni kwenye mikutano ya kampeni na alikuwa anaelekea Morogoro mjini.

Mafuwe alinusurika ajalini baada ya gari alilokuwa amepanda kugongwa nyuma na basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Arusha na Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, saa nane mchana katika Barabara Kuu ya Moshi kwenda Arusha maeneo ya uzunguni wilayani humo.

Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Tanga kwenda Arusha na mbunge alikuwa akienda maeneo ya uzunguni. Alipofika kona ya kuingilia kwa mkuu wa wilaya ndipo aligongwa na basi hilo ambalo lilikuwa linaelekea alikokuwa anaenda mgombea huyo wa ubunge.

Alisema mgombea huyo, wakati anakata kona kupanda kibao cha kuingilia nyumbani kwa mkuu wa wilaya basi hilo lilimgonga nyuma hivyo gari lake kupoteza mwelekeo na kupinduka mara tatu.

“Tunamshukuru Mungu mgombea ubunge hakuumia popote pamoja na walikuwamo ndani ya gari. Basi linashikiliwa kwa uchunguzi kubaini kama ajali hiyo imepangwa au ni bahati mbaya,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Sabaya ambaye ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama wilayani humo alisema ameviagiza vyombo vya usalama kuchunguza kwa kina tukio hilo ili kubaini kama linatokana na njama za kiasiasa au ni tukio la kawaida.