VIDEO: Profesa Kabudi aanika ubadhirifu ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema udhaifu mkubwa ambao umebainika katika balozi mbalimbali za Tanzania ni usimamizi wa fedha na mali katika balozi.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amewataka mabalozi watano walioapishwa leo Jumamosi Novemba 23, 2019 mjini Dodoma kusimamia vizuri fedha na mali katika nchi walizopangiwa.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa mabalozi hao Profesa Kabudi amesema udhaifu mkubwa katika balozi mbalimbali za Tanzania ni usimamizi wa fedha na mali huku akiutaja ubalozi wa Addis Ababa, Ethiopia.

“Waheshimiwa mabalozi mnakwenda lakini moja wa udhaifu mkubwa tulioubaini ni usimamizi wa fedha na mali katika balozi, ni udhaifu mkubwa, naomba muende  mkasimamie fedha na mali katika balozi.”

“Rais (John Magufuli) tumebaini baada ya kupata taarifa kutoka kwa balozi wetu wa Addis Ababa (Ethiopia), kumefanyika ubadhirifu na wizi mkubwa wa fedha katika ubalozi wetu huo.”

Amesema baada ya wizara kupata taarifa walipeleka  mkaguzi ambaye aliwasilisha ripoti na hatua za kisehria kuanza kuchukuliwa kwa waliohusika.

“Wizara ilichukua hatua mwezi wa kumi ya kumpeleka mkaguzi wa ndani kwenda kufanya ukaguzi na ameleta ripoti.”

“Ripoti imekabidhiwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa)  ili mwambata fedha aliyekuwa kabla ya kurejeshwa, hatua za kisheria zichukuliwe na tayari Takukuru wameshaanza zoezi hilo na mtu huyo yuko mikononi mwa Serikali,” amesema Kabudi

Mabalozi walioapishwa katika hafla hiyo na Rais Magufuli ni Meja Jenerali Anselm Shigongo Bahati (Misri), Mohamed Abdallah Mtonga (Abu Dhabi), Jestas Abouk Nyamanga (Ubelgiji),  Ali Jabir Mwadini (Saudi Arabia)  na Dk Jilly Elibariki  (Burundi).