Profesa Kabudi awapa mwezi mmoja mabalozi wapya

Tuesday January 14 2020

 

By Emmanuel Mtengwa na Harieth Makwetta, Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amewapa mwezi mmoja mabalozi wapya kuleta ripoti ya fursa zinazopatikana katika nchi wanazoenda kuwakilisha.

Pofesa Kabudi ametoa agizo hilo leo Jumanne Januari 14, 2019 katika hafla ya kuwaapisha mabalozi wateule wanne iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Profesa Kabudi ameanza kutoa agizo kwa balozi mpya wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliyemtaka kufuatilia taarifa ya maendeleo ya fursa ya ufundishwaji lugha ya Kiswahili nchini humo.

“Meja Jenerali Milanzi katika Jamhuri ya Afrika Kusini jambo kubwa ambalo Rais amelifanya wakati wa ziara yake kule ni kuhusu suala la ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili ambayo tayari Afrika ya Kusini wameshatangaza na wanaanza, fursa hiyo ilikuwa imepotea sana, fursa hiyo ilikuwa imetupita kwa sababu ya uzembe wetu wenyewe,” amesema

“Naomba utakapofika kituoni kazi ya kwanza, tafuta miadi ukukutane na waziri wa elimu wa Afrika Kusini ili jambo hilo likamilishe kabla ya mwezi wa pili tujue maendeleo ni nini,”

“Kama kuna lolote linalohitajika kutoka nyumbani tulifanye haraka sana ili juhudi aliyoifanya Rais Magufuli kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kuhusu Kiswahili tusifanye makosa tena kukosa fursa hiyo.”

Advertisement

Amesema waalimu wengi wa Kiswahili wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivyo balozi huyo afuatilie na kuleta taarifa ya makubaliano yaliyowekwa baina ya Rais wa Tanzania, John Magufuli na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.

Agizo lingine amelitoa kwa balozi mpya wa Tanzania nchini Namibia, Dk Modestus Kipilimba ambapo amemtaka kufuatilia makubaliano ya kibiashara ikiwamo biashara ya nyama na biashara ya kuwauzia Namibia nafaka

Pia, amemuagia balozi wa Zimbabwe, Profesa Emmanuel Mbennah kusimamia ushirikiano wa Zimbabwe na Tanzania wa fursa zilizopo za kibiashara.

“Dk (Benson) Bana unakwenda Nigeria, kufuatilie jinsi ya kushirikiana nao kwenye zao la korosho hasa jinsi ya kubadilishana uzoefu katika kilimo hasa kilimo cha korosho, kuongeza thamani ya korosho na kahawa, nitashukuru sana ukifuatilia hayo,” amesema Profesa Kabudi akimpa maagizo Dk Bana ambaye ameapishwa kuwa balozi mpya wa Nigeria

Amewataka mabalozi hao wapya wanne ndani ya mwezi mmoja baada ya kuwasili katika balozi walizopangiwa kuleta ripoti ya maeneo ya fursa katika nchi wanazowakilisha.

“Kama wote nilivyowaambia, ndani ya mwezi mmoja, nataka… nataka wala sio naomba, nataka ndani ya mwezi mmoja baada ya kuripoti vituoni mtuletee ripoti ya maeneo gani ya fursa tunayoweza kuyatumia” ameagiza

Mabalozi walioapishwa kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali ni pamoja na Meja Jenerali Gaudence Milanzi (Afrika Kusini), Dk Modestus Kipilimba (Namibia), Profesa Emmanuel Mbennah (Zimbabwe) na Dk Benson Alfred Bana (Nigeria)

Alichokisema Rais Magufuli

Mara baada ya kuawaapisha, Rais Magufuli amesema, “nchi tulizowapeleka ninyi wote wanne ni muhimu kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi yetu, sitazungumza sana tayari Waziri (Profesa Kabudi) amezungumza mengi lakini mimi ninawapongeze mnakwenda kufanya majukumu haya na mkayafanye vizuri kwelikweli kwa manufaa ya wananchi.”

“Kila nchi hapa ina umuhimu wake na waziri ameeleza Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe zote ni wanachama wa Sadc na mnafahamu mikakati ambayo tuliyonayo Sadc kwa sasa katika kujenga uchumi wa kisasa kasimamieni uchumi, kasimamieni Taifa.”

“Kahakikisheni mnatengenza ajira za Watanzania katika nchi mnazokwenda kuziwakilisha nina uhakika mkienda kusimama vizuri mtakwenda kufanya vizuri,” amesema Rais Magufuli.

Amesema maagizo hayo pia yanamhusu Balozi anayekwenda Nigeria, “Mungu ndiyo kila kitu nina imani kuwa mtafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.”

Katika kusisitiza Rais ameonya wale wenye tabia ya kupita maeneo mbalimbali kuaga wakishateuliwa kiasi cha kuchelewa katika maeneo yao ya kazi.

“Siku za nyuma kumekuwa na tabia mtu akishateuliwa ubalozi atakaa tena siku kadhaa anazunguka maofisi, anakuja kuaga kwa Rais, kwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri Mambo ya Nje, ataanza kwenda kwa wakurugenzi wa taasisi na wengine wanaanza kwenda mpaka kwa wakuu wa mikoa.”

“Mmeshateuliwa ninyi ni mabalozi nitaomba zile barua zao ziletwe mapema Waziri wa Mambo ya Nje ili ikiwezekana baada ya wiki moja au wiki mbili muwe mmeshaenda katika zile nchi ambazo mnatuwakilisha tunataka unapoteuliwa ni kuchapa kazi na hii ndiyo maana ya hapa kazi tu na mimi nina uhakika mtaweza,” amesema.

Advertisement