VIDEO: Profesa Kusiluka achambua wanaobeza wahitimu

Muktasari:

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Lugano Kusiluka amesema jitihada za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali zinahitajika ili kuondoa dhana inayojengwa kwamba wahitimu wengi hawawezi kuajirika.


Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini Tanzania wametakiwa kuungana pamoja kwa lengo la kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kiutendaji.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Septemba 19, 2019 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Lugano Kusiluka alipokuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi baada ya kutembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata relini.

Profesa Kusiluka alikuwa akifafanua uwepo wa malalamiko ya wahitimu wanaotoka vyuo vikuu kushindwa kutimiza majukumu yao kwa vitendo wanapokuwa wameajiriwa.

Amesema tatizo la wahitimu kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo lipo, lakini linapaswa kufanyiwa kazi kwa ushirikiano.

“Hili ni suala la ushirikiano kati ya taasisi ya elimu juu, Serikali, waajiri na wadau kutayarisha wahitimu wanaohitajika kwenye soko la ajira.”

“Kwa sababu mbali na jukumu la msingi la watoa elimu ikiwamo vyuo vikuu kuwafundisha kumekuwa na ugumu kwa  waajiri kuchukua wahitimu hao kuwapa mafunzo kwa vitendo kwenye ofisi, kampuni na taasisi zao, huku wakitarajia kupata wahitimu wanaojua kazi yao kwa vitendo,” amesema Profesa Kusiluka.

Amesema mbali na hilo ushirikiano huo uhamie kwenye kuwahamasisha wahitimu kujiajiri na kuzalisha ajira, badala ya kuwaza kuajiriwa.

“Kumekuwa na tabia ya wazazi kuwapangia watoto wao kozi za kusoma wakilenga kuajiriwa, bila kujua kuwa wanadumaza maono na ubunifu wa vijana hao.”

“Hivyo ni bora wakaachwa wasomee kitu wanachoona kwa wakati huo kinaweza kuwasaidia kuzalisha ajira badala ya kufikiria kuajiriwa, ”amesema Profesa huyo

Amesema kipindi cha udahili wazazi huwa wanapiga simu kuuliza watoto wao wasome kozi gani itakayowawezesha kupata ajira haraka.

Profesa huyo amesema kwa kulitambua hilo ndiyo maana Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Uganda na Kenya  wanatekeleza mradi wa kubadilisha uajiri kwa ajili ya maendeleo ya jamii, unaotekelezwa kwa miaka mitano.

Amesema kwenye mradi huo wanakusanya maoni ya waajiri, wanafunzi waliopo vyuoni, watu wa Serikali, walimu na wadau wa elimu kwa ujumla wakikusanya maoni ya kuboresha mitaala itakayotoa wahitimu wanaotegemewa na soko.

“Maoni hayo yanatumika kubadili mitaala mara kwa mara, lengo likiwa ni kupata wahitimu wanaohitajika sokoni na wanaomudu kufanya kazi walizozisomea kwa vitendo,” amesema.

Amesema hilo ndilo lililowafanya hata wakati dunia inahama kutoka kuwa na vyuo vya kitaaluma na kwenda vya watendaji  (critical thinkers) wao waliendelea kuzalisha wataalamu.

“Mzumbe bado tunazalisha wataalamu na tutaendelea kuwazalisha pamoja na mabadiliko hayo na nikikutana na watu wanaofanya nao wanasema wapo vizuri,” amesema Profesa Kusiluka.