Profesa Lipumba amlilia Mapalala

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kifo cha James Mapalala ni pigo kwa Taifa kwa kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa muasisi wa mageuzi nchini.

Geita. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kifo cha James Mapalala ni pigo kwa Taifa kwa kuwa mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa muasisi wa mageuzi nchini.

Mapalala amefariki dunia leo Jumatano Oktoba 23, 2019 katika Hospitali ya Kairuki alikokuwa akitibiwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Profesa Lipumba amesema Mapalala ni mwanzilishi wa chama cha CUF.

"Yeye na mzee Hamis Mlowo (marehemu) ndio waliokijenga na kukipa chama mizizi visiwani Zanzibar na Bara,  hata kauli mbiu yetu ya Haki inatokana na kazi yake.”

"Hata itikadi ya chama kuhakikisha tunatumia utajiri wa nchi kwa manufaa ya wananchi wote na katika uwanja wa siasa kutafuta demokrasia na kutafuta haki, Mapalala ameanza muda mrefu,” amesema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba amesema Mapalala aliwahi kuandika kuhusu watu kudai demokrasia na kusambaza andiko lake lililosababisha watu kukamatwa na kuwekwa ndani.

"Inapoandikwa historia ya kudai na kuleta demokrasia katika nchi huwezi kuliacha jina la James Mapalala. Litakuwa miongoni mwa majina hayo,” amesema Profesa Lipumba.

Amesema Mapalala aliondoka CUF na kwenda kuanzisha chama kingine baada ya kutokea hali ya sintofahamu katika chama hicho.

"Hata uchaguzi wa kwanza mwaka 1994 tuliweza kupata viongozi wa vijiji na madiwan  hasa jimbo la Kwimba ambako ilikuwa ngome yake,” amesema.

Mapalala aliyezaliwa Februari Mosi, 1936 ameacha mke na watoto kadhaa.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza waliojitosa kudai mfumo wa vyama vingi urejeshwe nchini Tanzania.

Kufuatia madai hayo, Mapalala alifungwa miaka miwili mkoani  Lindi kuanzia mwaka 1986 hadi 1989 na baada ya kutoka aliwekwa kizuizini kwa kipindi cha mwaka mmoja katika kisiwa cha Mafia baada ya  kuanzishwa chama cha siasa wakati sheria ilikuwa hairuhusu.

Alianzisha Chama cha Wananchi (CCW) mwaka 1991 na baadaye kiliungana na chama cha Zanzibar – Kamahuru na mwaka 1993 kuzaliwa Chama cha Wananchi (CUF).