MAHOJIANO MAALUMU: Profesa Mahalu aeleza siri ya urafiki na Mkapa

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (Saut)  Profesa Costa Mahula  akizungumza na waandishi wa gazeti hili jijini Mwanza. Pichana Johari Shania

Mwanza. Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu amefichua siri ya uhusiano wake na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa huku akisema alishawasamehe wote waliomwingiza katika kesi ya uhujumu uchumi.

“Kwangu binafsi, familia yangu, ukoo wote wa Mahalu na Watanzania wapenda haki; Mkapa alikuwa Rais, mzee wangu, rafiki na mtu mwema, mpenda haki na mtetezi wa wanaoonewa,” amesema Profesa Mahalu katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Mwanza hivi karibuni.

Profesa Mahalu ambaye kwa sasa ni makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Mwanza, alisema hayo alipokuwa akirejea kesi ya uhujumu uchumi iliyofunguliwa dhidi yake mwaka 2007.

Januari 22, 2007, Profesa Mahalu pamoja na aliyekuwa Ofisa Tawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Grace Martin walishtakiwa kwa madai ya kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania Italia.

Katika mchakato wa kesi hiyo, Mei 7, 2012, Rais mstaafu Mkapa aliandika historia baada ya kusimama kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwatetea washtakiwa hao, ushahidi ambao Mahalu anaamimi kwamba ndio uliomwezesha kuibwaga Serikali katika kesi hiyo.

Huku akiomba kutozungumzia zaidi kesi hiyo kwa sababu alishasamehe yote yaliyotokea, Profesa Mahalu alisema uamuzi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa wa kukubali kuwa shahidi wake mahakamani, ndio uliomwokoa.

“Kwangu hili la kesi lilishaisha. Nimeshamehe na roho yangu ni nyeupe,” alisema Profesa Mahalu.

“Pamoja na ukweli kwamba kesi ile iliharibu hadhi na heshima yangu, iliumiza na kuhangaisha familia yangu nilipohamishwa kutoka Roma, Italia wakati watoto wangu bado wanasoma; ilipoisha niliitisha misa ya shukrani na kusamehe yote,” alisema Mahalu.

Alisema ujio wa Mkapa mahakamani ulitimiza ahadi ya Mungu katika maandiko matakatifu ya Biblia kwenye Zaburi ya 17:2 inayosema “Katika matatizo yako, nitakuletea mashahidi wako.”

“Nitazidi kumshukuru Mzee Mkapa kwa uamuzi wake wa kuja mahakamani kunitetea. Alijua sina kosa na asingekuja ningeonewa sana,” alisema Mahalu.

Alisema ushahidi unaojitosheleza wa Mkapa ndio uliohitimisha kesi yake na kuifanya Serikali kuondoa kusudio la kukata rufaa dhidi ya ushindi alioupata katika hukumu iliyotolewa Agosti 9, 2012.

“Ilikuwa kesi ya uonevu kwa sababu aliyeifungua ndiye alikuwa msimamizi wa Wizara (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa) iliyosimamia mchakato na uamuzi wote. Lakini akiwa Rais akatengeneza kesi ambayo iliharibu hadhi yangu,” anasema Profesa Mahalu kwa tahadhari akikwepa kutaja majina ya wahusika.

Mahalu alishtakiwa wakati wa serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais, Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka kumi.

Alivyokomboa nyumba ya ubalozi

Profesa Mahalu alisema lipo jambo ambalo alilifanya akiwa balozi Italia mbalo halizungumzwi na kwamba ni vyema Watanzania wakalifahamu.

“Nilikomboa na kurejesha nyumba ya makazi ya Balozi, Italia iliyouzwa kinyemela,” anasema Profesa Mahalu.

Anaongeza, “kwa mwaka mzima wa mapambano mahakamani kurejesha jengo hilo, ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya hapa nyumbani ulikuwa duni. Ni Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilisaidia hadi shauri kumalizika haraka.”

Alisema kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa kesi za aina hiyo nchini Italia, shauri hilo lingechukua hata miaka 10 kumalizika endapo Serikali ya nchi hiyo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje isingeingilia kati.

“Jengo lile la balozi liliuzwa kinyemela na tayari mtu alishahamia anaishi kwa sababu mikataba ilimpa haki hiyo.

“Nililazimika kufungua shauri mahakamani kudai jengo lirejeshwe mikononi mwa Serikali ya Tanzania baada ya kubaini halikuuzwa kihalali,” alisema Balozi Mahalu.

Mwanadiplomasia huyo alisema katika kipindi chote kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea mahakamani, yeye na familia yake waliishi hotelini.

Alisema baada ya kushinda shauri mahakamani na kuamriwa jengo lirejeshwe kwenye miliki ya Serikali ya Tanzania, aliyeuziwa aligoma kutoka, hivyo Serikali ya Italia ikalazimika kutumia nguvu kumwondoa.

Alisema hata baada ya kupata msaada wa Serikali ya Italia kumtoa kwa nguvu aliyekuwa ameuziwa jengo hilo, kulikuwa na uwezekano wa mtu huyo kukimbilia mahakamani kukata rufaa na kuomba zuio la utekelezaji wa amri ya kumwondoa.

“Niliwaagiza maofisa wa ubalozi kupandisha mara moja Bendera ya Tanzania mara tu aliyeuziwa alipotolewa nje ili kuondoa uwezekano wa kesi nyingine, kwa sababu eneo lile tayari litakuwa ni ardhi ya Tanzania,” anasimulia na kuongeza.

“Hili la mimi kupambana hadi kurejesha jengo la makazi ya Balozi lililouzwa kinyemela halisemwi, isipokuwa lile la ofisi iliyokuwa na baraka za Serikali.”

Alisema baada ya jengo kurejeshwa, Rais John Magufuli (wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi) alilikarabati na kulirejeshea hadhi yake, kwani lilishaharibiwa vibaya na aliyeuziwa.

Anasema ukarabati huo ulirejesha ubora na hadhi ya jengo hilo ambalo anaamini bado linamilikiwa na Serikali ya Tanzania.

faa iliyokata kwa sababu isingekuwa jambo rahisi mbele ya macho ya sheria kung’ang’ania kesi inayohusu jambo ambalo Mkuu wa nchi ameshasema ilikuwa na baraka zake.

Asononeka wanafunzi wake kumshtaki

“Pamoja na maumivu ya kubambikiwa kesi ya kufunga, lakini pia niliumia na kushangazwa sana kuwa baadhi ya walionishtaki walikuwa wanafunzi wangu wa sheria pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),”

Hata hivyo, nguli huyo wa sheria aliyewahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria UDSM anasema aliwaelewa na kuwahurumia wanafunzi wake hao akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk Edward Hosea sababu walikuwa wanatekeleza maelekezo ya wakubwa wao.