Profesa Mbarawa ataka vyanzo vya maji kulindwa

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa  (kulia) akiagana na katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo baada ya kufungua mkutano wa Jukwaa la watumiaji maji jijini Dar es Salaam. Kushoto ni  Meneja Miradi wa 2030 Water Resources Group, Karin Maria Krchnak. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Waziri wa Maji nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amesema ni muda wa kuwekeza fedha kulinda vyanzo vya maji badala ya kujikita kuanzisha miradi.

Dar es Salaam. Waziri wa Maji nchini Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amesema ni muda wa kuwekeza fedha kulinda vyanzo vya maji badala ya kujikita kuanzisha miradi.

Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 3, 2019 wakati akifungua jukwaa la watumiaji maji nchini.

Amesema kuendelea kuanzisha miradi ya maji kila siku bila kutunza vyanzo vyake ipo siku watu watashtuka maji yameisha na wasijue cha kufanya.

"Ni wakati sasa wa kubadili mawazo yetu ya kubuni uanzishwaji miradi ya maji na badala yake tujikite katika miradi ya kutunza vyanzo vyetu vya maji kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa viwanda vya maji.”

"Ukweli ni kwamba maji hayaongezeki lakini watu wanaongezeka hivyo lazima vyanzo vya maji tulivyojaliwa tuvitumie kwa uangalifu na hili halitawezekana bila ya kuweka mikakati ya madhubuti ya kuvitunza," amesema Profesa Mbarawa.

Amesema baadhi ya maeneo kuna migogoro kutokana na uhaba wa maji akisisitiza kuwa  bila maji hakuna elimu, biashara wala ustaarabu.

Mwenyekiti wa jukwaa la maji, Mbogo Futakamba amesema jukwaa hilo ni la tatu kufanyika lengo likiwa kuweka mikakati ya matumizi shirikishi ya maji.

Mbogo ambaye ni katibu mstaafu Wizara ya Maji  amesema matumizi bora ya maji yatawezesha kuwa na uhakika wa chakula ikizingatiwa kuwa sasa kuna kilimo cha umwagiliaji.

Ofisa Maji  bonde la Wami/ Ruvu, Simon Ngonyani amesema jukwaa hilo lina faida kwa kuwa muda mrefu hakukuwa na ushirikishaji wa wadau katika utumiaji na utunzaji wa maji.