Profesa Mkumbo asema usanifu miradi ya maji Tanzania bado tatizo

Friday October 11 2019

By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Mtwara. Unyonge wa baadhi ya wahandisi kusanifu miradi ya maji vijijini unadaiwa kuwa chanzo cha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na wananchi kuendelea kukosa maji.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 na katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo katika uzinduzi wa jukwaa la wadau wa bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini.

Amesema kuna changamoto ya wataalamu kuwa na unyonge katika kutekeleza miradi na inapotumwa timu kufuatilia tatizo la kukwama inabainika shida ni kwenye usanifu.

"Usanifu sio jambo la kisiasa, sio jambo la wananchi, sio jambo la fedha ni jambo la utaalamu. Ni lazima kujiuliza tatizo ni nini kwa wahandisi wetu wa maji, hata katika ziara ya Rais (John Magufuli) changamoto iliyojitokeza ni miradi ya maji hasa vijijini ina changamoto,” amesema Profesa Mkumbo.

“Mtaalamu mzuri hatakubali kuharibu taaluma yake yuko tayari kupoteza cheo lakini atunze utaalamu wake. Hii  ni changamoto tunayokumbana nayo.”

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk Cosmas Masawe amewataka wananchi kuyatumia maji kujiletea maendeleo na kuzitaka taasisi zote kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi,  wahandisi kuzingatia mabadiliko hayo katika kufanya usanifu.

Advertisement

 


Advertisement