Profesa Mukandala aeleza mambo yaliyomchukiza Nyerere

Friday October 11 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Rwekaza Mukandala amesema kati ya mambo yaliyopigwa marufuku na mwalimu Julius Nyerere ni kutundika vyeti vya kitaaluma kwenye ofisi za umma.

Amesema marufuku hiyo ilifanya kuta za ofisini kutundika picha ya Rais na sio vyeti vya kitaaluma kama hapo awali.

Profesa Rwekaza ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 wakati akiwasilisha mada katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere linalofanyika UDSM.

"Jambo jingine alilopiga marufuku ni kuitwa majina ya vyeo alitaka majina kama ndugu, alikemea majivuno, ubadhilifu, dharau na uonevu," amesema.

Amesema Nyerere alikemea misafara mirefu ya viongozi, matumizi mabaya ya raslimali za umma na alitaka viongozi wasimamie haki na usawa.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema chuo hicho kinaandaa utaratibu wa kutoa orodha ya wananchi wa kwanza waliochangia ujenzi wake miaka 58 iliyopita.

Advertisement

"Mwalimu alikuwa na imani na wasomi, aliwaona wao kama chemchem ya fikra na alianzisha utaratibu wa kuzungumza na wanajumuiya, tuna kila sababu ya kumuenzi," amesema Prof Anangisye.

Kongamano la kumbukumbu ya mwalimu Nyerere linaendeshwa na Chuo cha Uongozi kwa ushirikiano na Kigoda cha Mwalimu cha Taaluma za Umajumui wa Afrika.

Advertisement