Profesa Ndalichako asikitishwa wanafunzi kupata daraja la nne, sifuri

Thursday October 17 2019

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kasulu. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Prosefa Joyce Ndalichako amesema Serikali imekuwa ikisikitishwa na baadhi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne na sifuri.

Amesema wanafunzi hao wamekuwa wakiiangusha Serikali baada ya kufanya vibaya katika matokeo yao ya kidato cha nne.

Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 17,2019 na wanafunzi wa shule ya sekondari Gugwe iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati wa mahafali ya 22 ya shule hiyo, Profesa Ndalichako amesema zawadi ya kuwapa wazazi na Serikali ni kusoma kwa bidii na kufaulu masomo yao.

Pofesa Ndalichako amesema Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa kuwekeza katika sekta ya elimu ambapo mpaka kufikia  Septemba 2019 imetumia Sh308 bilioni lakini wanafunzi wamekuwa wakishindishwa kufanya jukumu lao la kusoma kwa bidii.

"Serikali imekuwa ikisikitishwa na matokeo ya wanafunzi wanaokuwa wakipata daraja la nne na sifuri kwani imekuwa ikiwekeza nguvu nyingi katika miundombinu ya shule mbalimbali nchini jambo ambalo limekuwa likikatisha tamaa," amesema Profesa Ndalichako.

"Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa Watanzania wake na ndio maana inawekeza kiasi kikubwa cha fedha na kutegemea matokeo mazuri kwa wanafunzi," amesema Profesa Ndalichako.

Advertisement

Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange amesema kuchapwa fimbo kwa wanafunzi ni njia mojawapo ya kumfundisha na sio adhabu.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Kasulu Mji, Fatina  Laay  amesema wazazi waweze kufanya majukumu yao kwa watoto wao na kuacha kuwaozesha watoto wa kike kwa lazima kabla na baada ya kumaliza  shule ili waweze kujipatia kipato.

 

 

 

Awali, akisoma risala kwa niaba ya  wanafunzi shuleni hapo, Faraji Joseph amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali shuleni ikiwa ni pamoja na ukosefu wa uzio wa shule jambo linalowafanya kusoma kwa kuhofia usalama wao.

"Shule yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali pamoja na ukosefu wa maji na upungufu wa vifaa vya michezo, ambazo kama zitatatuliwa tutaweza kusoma kwa furaha na amani, "amesema Joseph.

Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1490 ambapo kati yao wanafunzi 172 watahitimu kidato cha nne mwaka 2019.


Advertisement