Profesa Ndalichako atoa siku 15 kwa mhandisi, mkandarasi wa JKT

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako

Muktasari:

  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako  ametembelea na kukagua miradi ya elimu katika shule ya sekondari Kigodya, Chuo cha ualimu Kabanga , shule ya sekondari Ruhita, Shule ya sekondari ya Nyantare ,Shule ya msingi Kasyenene, shule ya sekondari Kasangezi na chuo cha kilimo cha Bubondo wilayani Kasulu na kutoa maagizo.

Kasulu. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako ametoa siku 15 kwa mhandisi mshauri Fred Abel wa kampuni ya BICO na mkandarasi wa Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) wa mradi wa ujenzi wa chuo cha ualimu Kabanga kufanya mapitio upya ya kiasi cha fedha Sh10 bilioni walichoomba kwaajili ya ujenzi huo baada ya kutokuendana na mradi huo.

Mbali na kutoa siku hizo pia Profesa Ndalichako amesikitishwa na kasi ya ujenzi wa chuo hicho kilichopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma akisema umekuwa ukisua sua na kwenda taratibu jambo ambalo limekuwa likikwamisha wanafunzi kuhamia chuoni hapo.

Akizungumza jana Jumatano Oktoba 16, 2019 wilayani humo mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa majengo ya  chuo hicho alisema pamoja  na maagizo hayo pia ametaka kupatiwa gharama za ujenzi za kila jengo katika chuo hicho.

Profesa Ndalichako alisema ujenzi wa  majengo ya chuo hicho hauendani na kiasi hicho cha fedha ambazo tayari wameomba kwa serikali na kwamba tayari alishatoa agizo awali kuhusu kupitiwa upya kwa  gharama hizo lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa .

 

 

 

 

"Nilitamani chuo hiki kingewahi kumalizika haraka kwani majengo ya  chuo wanachosomea wanafunzi hao kwa sasa kipo hatarini kuwaangukia jambo ambalo ni hatari," alisema Profesa Ndalichako.

Mratibu wa mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu kutoka wizara hiyo, Ignas Chonya alisema anashindwa kuelewa kwa nini ujenzi huo umekuwa ukienda taratibu wakati fedha za ujenzi huo zipo na zimeshapitishwa tayari na serikali.

Awali, akitoa taarifa, Kaimu Mkuu wa Kanda ya ujenzi Luteni Kanali Onesmo Njau alisema chuo hicho chenye majengo 10, muda wa ujenzi ni miezi 15 na kwamba mpaka sasa umefikia asilimia 30.

Profesa Ndalichako yupo mkoani Kigoma kukagua miradi mbalimbali ya elimu katika halmashauri ya Buhigwe na Kasulu, ambapo miradi hiyo inatokana na fedha za mradi wa lipa kwa matokeo(EP4R).