RC Kigoma aeleza polisi walivyodhibiti ujambazi mkoani humo

Friday October 11 2019

By Anthony Kayanda, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Mkuu wa Mkoa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emanuel Maganga amesema kuanzishwa  kikosi maalum cha kupambana na ujambazi mkoani humo kimesaidia  wananchi kusafiri na kufanya kazi zao bila hofu ya kuvamiwa na majambazi.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 11, 2019 wakati akifunga kikao cha siku moja cha viongozi waandamizi wa polisi wa  Tanzania na Burundi kilichofanyika mjini Kigoma.

"Kuna wakati majambazi walikuwa wanafanya uhalifu hasa wilaya ya Kibondo na Kakonko  kiasi kwamba kuna wakati nikawa najiuliza hivi huu mkoa utatawalika kweli,” amesema Maganga.

Amesema alikaa na watendaji wengine kujadiliana kuhusu kuimarisha usalama mkoani Kigoma na hivi sasa hali ni shwari, hakuna matukio ya uhalifu kipindi cha nyuma.

"Miezi miwili iliyopita kuna tukio moja tu la uhalifu lililotokea mkoani Kigoma na polisi wetu walifanikiwa kuwadhibiti majambazi 12 licha ya kurushiana risasi kwa kipindi kirefu," amesema Maganga.

Amesema Tanzania na Burundi kuendeleza ushirikiano wa ulinzi katika mipaka ya nchi hizo lengo ni kupambana na ujambazi, hasa wanaofanya matukio hayo nchi moja na kukimbilia nchi nyingine.

Advertisement

Naibu mkurugenzi wa mashitaka wa Tanzania, Charles Kenyela amesema kupitia ushirikiano huo watahakikisha wanaondoa silaha zinazomilikiwa na watu kinyume na taratibu.

“Lengo ni kuona watu wanaishi bila hofu na kufanya shughuli zao za uzalishaji mali bila woga wa kuvamiwa na kuporwa mali na majambazi,” amesema Kinyela.

Advertisement