RC Kigoma aomba waziri aruhusu wanaume kuingia vyumba vya kujifungulia wanawake

Wednesday February 26 2020

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kibondo. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga amemuomba Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuruhusu wanaume ambao wake zao wanaenda kujifungua waingie nao kwenye vyumba vya kujifungulia kwani itasaidia kupanga idadi ya watoto wanaowakata na kuleta mshikamano kwenye familia. 

Akizungumza leo Jumatano Februari 25, 2020 katika Chuo cha Uuguzi na Ukunga kilichopo wilayani hapa amesema ni wakati sasa kwa wizara husika ikaruhusu jambo hilo kwani kuna baadhi ya nchi tayari wanao utaratibu huo na kwamba hata ndugu wa karibu wa mama mjamzito pia wapewe ruhusa hiyo.

Amesema hatua hiyo itapunguza malalamiko kwa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya watumishi wa sekta ya afya kwa kuwanyanyasa na kutoa lugha za matusi kwa kina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

"Namuomba waziri suala hili lifanyike kwa nguvu kubwa kwani wazazi wa kiume wakiingia katika chumba cha kujifungulia wenza wao jambo hilo litaleta mshikamano kwenye familia hiyo na kupanga idadi ya watoto wao," amesema Maganga.

Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Sarafina Simon amesema kabla ya kuwepo kwa jengo hilo wamekuwa wakienda nje ya chuo hicho kujifunza mafunzo ya vitendo lakini baada ya kukamilika itasaidia kusoma kwa utulivu na umakini kuliko awali.

Amesema jengo hilo litasaidia wao kufanya vizuri katika masomo yao kwani lina vyumba vya kutosha na vifaa tofauti na jengo walilokuwa wanalitumia awali.

Advertisement

Advertisement