RC Kilimanjaro afanya ukaguzi makanisani

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira akiwa katika ziara ya kushtukiza katika Kanisa la TAG,Kilimanjaro Revival Temple Moshi Mjini. Picha na Janeth Joseph

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amefanya ziara ya kushtukiza katika makanisa mbalimbali ya Mkoa huo ambapo amekuta baadhi ya makanisa hayajazingatia agizo la Serikali la kumtaka kila muumini kukaa usawa wa mita moja na mwenzake  kufuatia ugonjwa wa corona.
Mghwira alianza ziara hiyo asubuhi ya Machi 29, 2020 na kukagua makanisa mbalimbali kama yamezingatia agizo la serikali la watu kutogusana ambapo aliagiza viongozi wa makanisa kuendelea kutoa elimu kwa waumini  namna ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Makanisa ambayo yalikaguliwa ni Kanisa Kuu  Katoliki la Kristu Mfalme Jimbo la Moshi, Kanisa la TAG, Kilimanjaro revival temple Moshi Mjini, Kanisa la Anglikana la St.Margaret's pamoja na Kanisa la KKKT usharika wa Moshi mjini ambapo kila kanisa liliweka maji pamoja na vitakasa mikono kwenye milango ya kuingia kanisani.
Akizungumza na waumini wa makanisa hayo  aliwataka wazingatie maagizo yanayotolewa na Serikali kwa ufasaha ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo  pamoja na  kuhakikisha wanafunga na kuomba na kusema kuwa mpaka sasa mkoa huo uko salama kwani wasafiri wote walioingia nchini wako salama na kwamba hakuna aliyegundulika kuwa na maambukizi.
''Naamini mkoa wetu utashinda maana mpaka sasa hakuna maambukizi ,wasafiri wote wanaoingia kutoka nje ya nchi wako salama na sisi tunafuatilia kwa karibu sana,'' amesema Mghwira.
''Mikusanyiko ya rohoni tunajua ina nguvu mara dufu ya mikusanyiko hii, lakini mikusanyiko hii ya sasa ni kwasababu tuu ya utu, kuna sehemu ndani ya makanisa watu wamekaa mbalimbali na wengine hawajazingatia hilo, naombeni mzingatie yale mnayoelekezwa ili tujihadhari na ugonjwa huu,"
''Lakini endapo ibilisi atajiingiza katika ugonjwa  na ikabidi tubanane nyumbani basi mikusanyiko ya rohoni na itawale ,kwa vyovyote vile tuhakikishe mwovu hatushindi lakini tumshinde kwa kutunza miili yetu,''amesema Mghwira
Rony Swai mchungaji Mkuu wa TAG, Kilimanjaro revival Temple, amesema wameweka utaratibu wa kufunga na  kuomba kila Ijumaa kwa ajili ya kuliombea Taifa mpaka siku watakaposikia ugonjwa huo umeisha.