RC Lindi ahamasisha wananchi kujiandikisha

Monday October 14 2019

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka wananchi wa Mkoa huo kutumia siku tatu zilizoongezwa na Serikali kujiandikisha uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesema katika siku hizo zilizoongezwa hadi Oktoba 17, 2019 wananchi wanatakiwa kuzitumia kikamilifu kujiandikisha.

Amebainisha kuwa mkoani humo hadi jana Jumapili Oktoba 13, 2019 watu 327,280 walikuwa wamejiandikisha kati ya 557,825.

Ameeleza hayo katika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge yanayofanyika mkoani Lindi sambamba na kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere.

Amesema watakaozitumia siku hizo tatu watakuwa wametimiza haki yao ya msingi ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

Kuhusu elimu,  Zambi amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo sasa ni mimba kwa wanafunzi.

Advertisement

Amesema wanaendelea kushirikiana na mahakama kuwachukulia hatua wanaowapa mimba wanafunzi.

“Tunaendelea na operesheni kuhakikisha wanaowakatisha wanafunzi masomo  kwa kuwapa  mimba tunapambana nao,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa upande wa ufaulu, Zambi amesema Lindi ndio Mkoa pekee ambao haukuwa na daraja sifuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita na wanafunzi sita tu walipata daraja la nne.

“Kwenye ufaulu nataka niseme kwa miaka mitatu mkoa wa Lindi umefanya vizuri matokeo ya kidato cha sita, na sasa hizi tumesema lazima tuendelee kufanya vizuri,” amesema Zambi.

Advertisement