RC Makonda afichua siri ya kusaidia watoto mara kwa mara

Friday December 6 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema kila mara amekuwa akijitahidi kutafuta watu wa kutoa msaada wa matibabu kwa watoto wanaousumbuliwa na matatizo ya moyo kwa sababu anajua uchungu wa kuishi bila mtoto.

Makonda ameyasema hayo leo, Disemba 5, 2019, alipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ili kushuhudia upasuaji kwa watoto walio na matatizo ya moyo unavyofanywa na madaktari bingwa wa Tanzania, wakishirikiana na madaktari bingwa wa matatizo ya moyo wa King Salman humanitarian Aid and Relief Centre wa nchini Saudi Arabia.

Makonda aliyekuwa ameongozana na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia, Mohamed bin Mansour Al-Azizi, amesema kwa miaka saba aliyokaa katika ndoa na mkewe bila kujaliwa kupata mtoto alikuwa akishuhudia jinsi anavyohangaika kutafuta mtoto jambo ambalo lilikuwa likimtia huzuni.

 

“Najua jinsi nyumba ikiwa haina mtoto inavyokuwa na sasa naona furaha tuliyo nayo ndani ya nyumba baada ya kupata mtoto, jambo hili limekuwa likinifanya mimi kuhangaika kila kona kutafuta watu wanaoweza kutoa msaada wa matibabu kwa watoto walio na matatizo ya moyo,” amesema Makonda.

Amesema kitendo kilichofanywa na Saudi Arabia kuleta wataalamu ili kusaidia kufanya upasuaji wa kibingwa kwa watoto hao, kinaonyesha mapenzi ya dhati na utu walio nao kwa Watanzania tofauti na wengine.

Advertisement

“Wamejitoa kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa watu wasio na uwezo wa kugharamia matibabu hayo huu ni upendo mkubwa na siyo wanaipenda Tanzania tu, bali na watu wake kwa sababu unaweza kupenda Tanzania kwa ajili ya biashara, lakini hawa wanaipenda Tanzania na watu wake,” amesema mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi amesema katika kambi hiyo ya upasuaji,  watoto 64 wenye matatizo ya moyo wamefanyiwa upasuaji mkubwa na mdogo.

Upasuaji huo wa bure uliofanywa na madaktari hao kuanzia Desemba 1 hadi 5, ungegharimu Sh465.06 milioni kama wagonjwa hao wangetakiwa kuyalipia matibabu hayo.

Profesa Janabi amesema katika idadi ya watoto ambao wamepatiwa huduma, 24 walifanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua huku wengine wakifanyiwa upasuaji mdogo wa kuziba matundu katika moyo.

“Na leo madaktari hawa wamepanga kuhudumia kati ya watoto 5 hadi 6, idadi inayoweza kuongezeka zaidi ya hapo kwa sababu uhitaji bado ni mkubwa na sisi tunaendelea kuhakikisha tunawafikia wote wenye uhitaji.”

“Mpaka sasa bado tuna wagonjwa 50 wanasubiri operesheni ambao tutaendelea kuwahudumia,” amesema Profesa Janabi.

Kiongozi wa ujumbe wa madaktari hao, Dk Loay Abdulsamad amesema katika upasuaji huo madaktari wa ndani walifanya kazi kuwa rahisi kutokana na kushiriki kikamilifu katika shughuli nzima kwa zaidi ya asilimia 80.

“Ni mara yetu ya kwanza kuja Tanzania na tumefurahi kuwa hapa kutokana na ushirikiano tulioupata, tutafanya kila tunaloweza ili mwakani tena tuje kusaidia watu wenye uhitaji.” Amesema Dk Loay

Advertisement